NA CHAUSIKU SAID
MATUKIO DAIMA MEDIA ,MWANZA.
Jeshi la Polisi Mkoa wa Mwanza linamshikilia Richard Jackson (miaka 38), machinga mkazi wa Kageye, Kata ya Lwanhima, Wilaya ya Nyamagana kwa tuhuma za kupatikana na noti bandia.
Akizungumza na waandishi wa habari, Kamanda wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Mwanza Wilbroad Mtafungwa ameeleza kuwa jeshi la polisi lilipata taarifa juu ya kuonekana kwa mtuhumiwa huyo akiwa na fedha bandia za kigeni na za Tanzania.
“Baada ya kupatiwa taarifa hizo tuliandaa mpango kazi na ukafanikiwa kumkamata mtuhumiwa akiwa na noti bandia za Tsh 10,000 noti 646 zenye thamani ya Tsh milioni sita laki nne na sitini, noti za Tsh 5,000 zilizokamilika 602 zenye thamani ya Tsh milioni tatu na elfu kumi, huku ambazo hazijakatwa zikiwa 490 zenye thamani ya Tsh milioni mbili laki nne na elfu hamsini,” alisema Kamanda Mtafungwa.
Mtafungwa, ameeleza kuwa mtuhumiwa huyo alikutwa pia na noti za Tsh 2,000 zikiwa 96 zenye thamani ya laki moja na elfu tisini na mbili pamoja na noti ya Tsh 1,000 moja.
Jumla ya noti zote zilizokamatwa ni 2,691 zilizokadiriwa kuwa na thamani ya Tsh milioni thelathini na saba, laki mbili, arobaini na mbili elfu, mia tano kumi na nne na senti hamsini na sita.
Hata hivyo, jeshi la polisi limefanikiwa kukamata vitendea kazi vinavyotumika kuchapisha fedha hizo bandia vikiwemo mtambo wa kutengeneza fedha (printer machine) aina ya EPSON, pasi ya Kijerumani yenye chapa ya Simba, rangi mbalimbali za kuchanganyia, laptop moja, sanduku la mbao, rim mbili za karatasi (moja ikiwa imetumika) pamoja na laini nne za simu za mitandao tofauti.
Jeshi la Polisi linaendelea na uchunguzi kwa kushirikiana na taasisi nyingine ili kuweza kubaini mtandao wa wahalifu hao.
Mtuhumiwa Richard Jackson anashikiliwa kwa mahojiano zaidi. Aidha, jeshi la polisi linatoa wito kwa wananchi kuongeza umakini hasa kwenye matumizi ya fedha ili kubaini uwepo wa fedha bandia na kuendelea kutoa taarifa za wahalifu na uhalifu ili ziweze kufanyiwa kazi kwa haraka.
0 Comments