Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi, ametunuku Nishani ya Mapinduzi pamoja na Nishani ya Utumishi Uliotukuka kwa viongozi na wananchi mbalimbali wenye sifa maalum, waliotoa mchango mkubwa katika historia, maendeleo na ustawi wa Zanzibar.
Akisoma Tamko la Kwanza la Kutunuku Nishani hizo, Katibu Mkuu wa Afisi ya Rais, Ikulu Zanzibar, Ndg. Saleh Juma Mussa, amesema jumla ya watu 18 wametunukiwa Nishani hizo, ikiwa ni sehemu ya kutambua mchango wao wa kipekee kwa Taifa.
Hafla hiyo imefanyika leo, tarehe 11 Januari 2026, katika Viwanja vya Ikulu, Mnazi Mmoja Zanzibar, na imehudhuriwa na viongozi wa kitaifa, viongozi wa vyama vya siasa, watendaji wakuu wa taasisi za umma, wakuu wa vikosi vya ulinzi na usalama, pamoja na wananchi mbalimbali. Tukio hilo ni miongoni mwa shamrashamra za Maadhimisho ya Miaka 62 ya Mapinduzi ya Zanzibar ya mwaka 1964.
Waliotunukiwa Nishani ya Mapinduzi ni pamoja na:
1. Mama Fatuma Karume – Mjane wa Rais wa Kwanza wa Zanzibar
2. Mufti Mkuu wa Zanzibar, Sheikh Saleh Bin Omar Bin Kaab Bin Ahmed Baalawiy
3. Marehemu Sheikh Hassan Bin Ameir Al-Shirazy
4. Marehemu Sheikh Mussa Makungu Ali
5. Marehemu Askofu John Ackland Ramadhani
6. Profesa Jose Piquer
7. Ndugu Gulam Abdalla Rashid
8. Marehemu Bimvita Mussa Kibendera
Waliotunukiwa Nishani ya Utumishi Uliotukuka ni pamoja na:
9. Brigedia Jenerali Said Hamis Said
10. Kamishna wa Polisi (CP) Kombo Khamis Kombo
11. Kamishna wa Uhamiaji (CI) Hassan Ali Hassan
12. Commodore Azana Hassan Msingiri
13. Kanali Makame Abdallah Daima
14. Kamishna Rashid Mzee Abdallah
15. Kamishna Khamis Bakari Khamis
16. Kanali Burhani Mzee Nassor
17. Luteni Kanali Said Ali Shamhuna
18. Ndugu Ali Abdalla Ali
Nishani ya Mapinduzi hutolewa kwa mtu aliyeasisi, kushiriki au kuyatukuza Mapinduzi ya Zanzibar ya mwaka 1964, au kwa kiongozi, mtu aliye hai au aliyefariki aliyeiletea Zanzibar heshima na sifa katika fani mbalimbali, pamoja na kuonesha maadili mema yanayostahili kuigwa.
Kwa sasa, Wazanzibari wanaendelea kuadhimisha Miaka 62 ya Mapinduzi ya Zanzibar kupitia shamrashamra na matukio mbalimbali, ikiwemo ufunguzi na uzinduzi wa miradi ya maendeleo, kuelekea kilele cha Siku ya Mapinduzi tarehe 12 Januari 2026.














.jpg)















0 Comments