Na Hamida Ramadhan,Matukio Daima Media Dodoma
ZAIDI ya wasichana 300 waliopata mimba wakiwa na umri mdogo (Young Mothers) wamewezeshwa kupitia mradi wa "Kijana Imara" unaotekelezwa na taasisi ya Restless Development Tanzania kwa ufadhili wa Shirika la Maendeleo la Uswisi (Swiss Agency for Development and Cooperation – SDC) kupitia Shirika la Umoja wa Mataifa la Idadi ya Watu (United Nations Population Fund – UNFPA).
Mradi huu unatekelezwa Tanzania Bara na Visiwani, na kwa sasa unatekelezwa katika mkoa wa Dodoma kwenye wilaya tano ambazo ni Dodoma Mjini, Chamwino, Kongwa, Bahi na Kondoa DC.
Wasichana hao walipewa mafunzo ya ujuzi wa maisha, elimu ya afya ya uzazi, na ujasiriamali ambapo baada ya mafunzo, walipewa vifaa vya kazi ikiwemo mashine za kushona nguo (chelehani), vifaa vya saluni, na mabanda ya kisasa ya kufugia nguruwe.
Akizungumza wakati wa ugawaji wa vifaa hivyo, Afisa Mradi wa Restless Development Tanzania, Ally Saad, alisema taasisi yao inalenga kuwawezesha vijana hasa wasichana waliopata mimba wakiwa shuleni kujitambua na kujikwamua kiuchumi na kijamii.
“Wasichana hawa mara nyingi hutengwa na jamii na familia zao baada ya kupata mimba wakiwa na umri mdogo. Tunawapa elimu, tunawajengea ujasiri na kuwasaidia kurejesha ndoto zao,” alisema Saad.
Mradi pia unashirikiana na Halmashauri za Wilaya kuwaunganisha wasichana katika vikundi ili waweze kufaidika na mikopo ya asilimia 10 ya mapato ya ndani ya Halmashauri kwa wanawake, vijana na watu wenye ulemavu.
Kwa kushirikiana na CRDB Bank Foundation, wasichana hupatiwa elimu ya fedha na baadaye kupewa mtaji kulingana na shughuli wanayopenda kufanya kama vile ushonaji, mapishi, saluni au ufugaji.
Lengo la mradi huu ni kuwakinga dhidi ya kupata mimba ya pili kwa kuwawezesha kuwa na kipato, hali itakayowapa uwezo wa kufanya maamuzi sahihi kwa ajili ya maisha yao na familia zao.
Kwa upande wao Vijana waliopata mafunzo na vifaa vya kuanzisha shughuli za kiuchumi kupitia mradi wa Kijana Imara, unaotekelezwa na Restless Development Tanzania kwa ufadhili wa Shirika la Maendeleo la Uswisi (SDC) kupitia Shirika la Umoja wa Mataifa la Idadi ya Watu (UNFPA), wamehimizwa kutumia kwa uangalifu fursa waliyopewa ili kujiinua kiuchumi na kijamii.
Akizungumza katika hafla ya kugawa vifaa hivyo, Veronica Baluwa-Afisa maemdeleo jamii kata ya Buigiri aliwataka vijana hao kuchukulia msaada waliopata kama mtaji wa maisha, huku akisisitiza kuwa kuna wengine wengi wanaowaangalia kuona mafanikio yao
"Mmetunukiwa fursa ambayo si kila mmoja ameipata. Hakikisheni ndani ya miezi sita mnaanza kuonyesha mafanikio, fanyeni kazi kwa bidii ili mje kuwa mfano kwa vijana wengine,” alisema mtendaji huyo.
Nekiweti Gayewi-Afisa maendelea Chamwino aliwahimiza pia kuhakikisha wanadhamini na kuthamini kila walichopewa kama vile wametolea jasho lao wenyewe, na kuonya dhidi ya kutoitumia fursa hiyo kwa makusudi au uzembe
.“Vitendea kazi hivi ni mwanzo wa mabadiliko katika maisha yenu. Thamini msaada huu kama umeupata kwa gharama zako binafsi,” aliongeza Afisa maendeleo huyo.
Kwa upande wake, mzazi wa mmoja wa wasichana walionufaika, aliyejulikana kwa jina la Mama Nyemo alisema anaamini kuwa fursa aliyopata binti yake ni njia ya kumtoa kwenye utegemezi.
“Ninamshauri mwanangu afanye kazi kwa moyo mmoja, hasa kazi ya mikono kwenye saluni aliyofundishwa. Ni matumaini yangu kuwa kazi hii itamsaidia kulea mtoto wake bila kuwa tegemezi tena,” alisema mzazi huyo kwa furaha mama Nyemo
Naye Mariam Dicksonmnufaika,anatokea chamwinoa akiongea kwa niaba ya Wasichana waliopata mafunzo hayo wameishukuru taasisi hiyo kwa kuwakumbuka wasichana .
"Tumekabidhiwa vifaa mbalimbali kama vile mashine za kushonea (chelehani), vifaa vya saluni, mabanda ya kufugia kuku pamoja na elimu ya fedha, uzazi wa mpango, ujasiriamali na uongozi tunaahidi tunakwenda kufanya kazi kwa bidii tulndokane na utegemezi uliokuwa huko nyuma, " Amesema
Mradi wa Kijana Imara umelenga kuwainua wasichana waliopata ujauzito wakiwa shuleni kwa kuwapatia elimu ya maisha, afya ya uzazi, ujasiriamali na mitaji midogo ya kuanzisha biashara, ili kuwawezesha kujiamini, kujitegemea na kuchangia maendeleo ya jamii.
0 Comments