Header Ads Widget

MAZUNGUMZO YA KUSITISHA MAPIGANO GAZA YANAKARIBIA KUSAMBARATIKA, MAAFISA WA PALESTINA WANASEMA

 

Mazungumzo kati ya Israel na Hamas nchini Qatar kuhusu mpango mpya wa kusitisha mapigano Gaza na kuachiliwa kwa mateka yanakaribia kusambaratika, kwa mujibu wa maafisa wa Palestina wanaofahamu undani wa majadiliano hayo.

Afisa mmoja mwandamizi aliiambia BBC kwamba Israel "ilipoteza muda" wakati wa ziara ya Waziri Mkuu Benjamin Netanyahu mjini Washington wiki hii na kwa makusudi kusimamisha mchakato huo kwa kutuma ujumbe wake Doha wasio na mamlaka ya kufanya maamuzi kuhusu mambo muhimu katika mzozo huo.

Masuala hayo ni pamoja na kuondolewa kwa wanajeshi wa Israel na usambazaji wa misaada ya kibinadamu.

Kabla ya kuondoka Marekani siku ya Alhamisi, Netanyahu alikuwa ameonyesha mwitikio chanya, akisema anatumai kukamilisha makubaliano "katika siku chache zijazo".

Alisema mpango uliopendekezwa utaifanya Hamas kuachilia nusu ya mateka 20 hai ambao bado inawashikilia na zaidi ya nusu ya mateka 30 waliokufa wakati wa mapatano yaliyodumu kwa siku 60.

Tangu Jumapili iliyopita, wapatanishi wa Israel na Hamas wamehudhuria duru nane za mazungumzo katika majengo tofauti huko Doha.

Wamewezeshwa na Waziri Mkuu wa Qatar Sheikh Mohammed bin Abdul Rahman Al Thani na maafisa wakuu wa kijasusi wa Misri, na kuhudhuriwa na mjumbe wa Marekani Brett McGurk.

Wapatanishi hao wamewasilisha makumi ya ujumbe wa maneno na maandishi kati ya ujumbe wa Hamas na wa Israel, ambao umejumuisha masuala ya kijeshi, usalama na kisiasa.

Lakini siku ya Ijumaa usiku, maafisa wa Palestina wanaofahamu mazungumzo hayo waliiambia BBC kwamba yalikuwa yakikaribia kusambaratika, huku pande hizo mbili zikiwa zimegawanyika sana katika masuala kadhaa yenye utata.

Jeshi la Israel lilianzisha kampeni huko Gaza kujibu shambulio lililoongozwa na Hamas kusini mwa Israel tarehe 7 Oktoba 2023, ambapo takriban watu 1,200 waliuawa na wengine 251 walichukuliwa mateka.

Takriban watu 57,823 wameuawa huko Gaza tangu wakati huo, kulingana na wizara ya afya ya eneo hilo inayoendeshwa na Hamas.

Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI