Header Ads Widget

MAANDAMANO KENYA: MAMA AOMBOLEZA MWANAWE ALIYEPIGWA RISASI AKIWA ANATAZAMA RUNINGA

 

Siku ya Jumatatu, wakati maandamano ya kupinga serikali yalipokuwa yanaenea katika maeneo mengi nchini Kenya, Bridgit Njoki mwenye umri wa miaka 12 alikuwa ameketi akitazama televisheni katika nyumba yao kama kawaida.

Hakujua kwamba mapigano makali yaliokuwa yakiendelea kati ya waandamanaji na polisi wenye silaha angekutana nayo sebuleni kwao.

Risasi moja ilipenya kwenye paa ya nyumba yao, ikatoboa dari na kumpiga Njoki kichwani, mamake Lucy Ngugi, alisema na ndani ya masaa machache, alitangazwa kuwa amefariki dunia akiwa hospitalini.

"Alikuwa kila kitu kwangu," Bi Ngugi alisema, alipokuwa akilia nyumbani kwake nje kidogo ya jiji la Nairobi. "Alikuwa muhimu sana kwangu."

"Niwe mama wa mwisho kulia kwa kifo cha mtoto. Mtoto asiye na hatia. Natamani hata angekuwa anacheza nje ... lakini ndani ya nyumba? Ee Mungu wangu, hii ni uchungu."

Njoki ni mmoja wa waathiriwa wenye umri mdogo zaidi wa ghasia zilizokumba Kenya katika muda wa mwezi mmoja uliopita.

Kulingana na Tume ya Kitaifa ya Haki za Kibinadamu ya Kenya (KNCHR), karibu watu 70 wamefariki na mamia kujeruhiwa katika maandamano matatu makubwa ambayo yamefanyika tangu Juni 17.

Maandamano hayo ambayo kwa kiasi kikubwa yanaongozwa na vijana- yanaakisi kutoridhika juu ya masuala kama vile gharama ya maisha, kupanda kwa ushuru, deni kubwa la umma, na ukatili wa polisi.

Mnamo tarehe 7 Julai, siku ambayo Njoki alikufa, mamlaka ilifunga barabara kuu kwa ajili ya maandalizi ya kukabiliana na maandamano.

Ushahidi wa video unaonyesha polisi wakifyatua vitoza machozi, na katika visa vingine, wakifyatua risasi katika maeneo ya makazi ambapo waandamanaji walikuwa wanatawanywa kisha wanakusanyika tena.

"Risasi ilipitia juu ya paa la nyumba na ikatoboa dari, pale ambapo Njoki alikuwa ameketi kwenye kiti," alisema bibi yake Njoki, Margaret Njeri.

"Ghafla, mama yake alimbeba na kuja naye nyumbani kwangu huku akiwa anapiga mayowe: 'Mama, mtoto wangu amepigwa risasi!' Sikuweza hata kumshika mtoto."

Risasi iliyompata Njoki iliingia kupitia paa la nyumba na kutoboa dari

Familia hiyo ilifikiri kuwa iko mbali na mapigano hayo makali, ikizingatiwa kuwa wanaishi Ndumberi, kijiji kilicho karibu kilomita mbili (maili 1.2) kutoka barabara kuu.

"Nilikuwa na uhakika ni risasi," mamake Njoki anasema. "Mshindo uliosikika kwenye paa ulikuwa mkubwa sana."

Polisi wametupilia mbali madai ya familia hiyo, wakisisitiza kwamba risasi haingeweza kutoka barabara kuu hadi nyumbani kwao. Lakini mwili wa Njoki ambao hauna uhai tena unatoa taswira tofauti.

Ripoti ya uchunguzi wa mwili wa mtoto huyo wa miaka 12 inasema madaktari walipata risasi kutoka kwenye mwili wake, na kwamba jeraha lake la kichwa "lilifanana na risasi".

Njoki alikuwa mwanafunzi wa darasa la 7 katika Shule ya Benson Njau huko Ting'ang'a, kijiji jirani na eneo lao. Akiwa mzaliwa wa kwanza wa familia, alikuwa akisaidia kutunza wengine, kazi za nyumbani, na fahari ya nyumba yao.

"Daima alikuwa nambari moja katika darasa lake," bibi yake anasema. "Mtiifu na nadhifu sana.

"Hata kwa jinsi alivyozungumza. Alikuwa msichana mzuri sana. Alipenda sana kuhudumu kanisani. Alisaidia ndugu zake. Alinipikia. Alikuwa kila kitu."

Mamake Njoki anamtaja kama "msichana mzuri, mrembo, ambaye alikuwa na ndoto nyingi".

Baba yake ameumia sana, ameshindwa hata kuzungumza kuhusu msichana wake. Ndugu zake pia wako kimya. Huzuni imetanda huku kiti cha Njoki kikiwa bila mtu.

Vifo vya watu kadhaa kama Njoki vimesababisha shutuma kimataifa.

Umoja wa Mataifa ulisema umesikitishwa sana na mauaji hayo na kukosoa polisi kwa kutumia "risasi za kuua" dhidi ya waandamanaji.

Matukio haya yote ni kama marudio ya mwaka jana, ambapo kulingana na Shirika la kutetea haki za binadamu nchini Kenya (KNCHR), zaidi ya watu 50 walikufa katika msako wa polisi uliofanywa kwa miezi kadhaa kwa sababu ya maandamano ya kupinga serikali.

Rais Ruto amechukua msimamo mkali haswa wakati huu.

Katika hotuba kwa taifa kufuatia maandamano ya Julai 7, ambapo watu 38 waliuawa, kwa mujibu wa tume ya serikali ya haki za binadamu, Ruto alisema: "Yeyote atakayepatikana akichoma biashara au mali ya mtu mwingine apigwe risasi mguuni, alazwe hospitalini na baadaye afikishwe mahakamani. Msiwaue, lakini hakikisheni mumewavunja miguu."

Vile vile, Ruto amewashutumu wapinzani wa kisiasa kwa kuchochea ghasia kwa nia ya kumng'oa madarakani kinyume cha sheria, lakini wapinzani wa rais wamepuuzilia mbali madai hayo.

Wakati huo huo, katika eneo la Ndumberi, familia ya Njoki inaomba tu kukomeshwa kwa ukatili huo.

"Nitamzika Njoki, lakini sitasahau kamwe Siku ya Saba Saba [7 Julai]. Acha Njoki awe wa mwisho kufa kwa sababu ya maandamano," mamake anasema.

Maandamano ya kupinga serikali yanayoendelea yamebadilisha siasa za Kenya. Yanataka uwazi, uelewa na kusikilizwa. Lakini gharama yake imekuwa damu kumwagika.

Na wakati ghasia zikiendelea, jina la Njoki na wengine wengi waliopoteza maisha yao yamekuwa kama ishara- ya kutokuwa na hatia, unyanyasaji wa serikali, na ukosefu wa uwajibikaji.

"Tusichome nchi yetu. Tufanye mazungumzo. Tuzungumze. Sisi ni kaka na dada, naiomba serikali yetu - hii isitokee kwa mzazi mwingine yeyote," mamake Njoki anasema.

"Mtoto mwingine asife kama Njoki."

Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI