Na Hamida Ramadhan, Matukio Daima Media Dodoma
MAKAMU wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika Kongamano la Kitaifa la Mashirika Yasiyo ya Kiserikali (NGOs) linalotarajiwa kufanyika kuanzia tarehe 11 hadi 13 Septemba 2025, jijini Dodoma.
Kongamano hilo linaandaliwa na Ofisi ya Msajili wa Mashirika Yasiyo ya Kiserikali Tanzania Bara, kwa kushirikiana na mitandao ya NGOs nchini, na litawakutanisha zaidi ya mashirika elfu moja kutoka maeneo mbalimbali ya Tanzania.
Akizungumza kuhusu maandalizi ya kongamano hilo, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Bi. Felister Mdemu, alisema kongamano hilo ni sehemu ya tathmini ya miaka mitano ya utekelezaji wa kazi za NGOs, ambapo mashirika yatapima mafanikio, changamoto na mchango wao kwa jamii katika maeneo kama afya, elimu, jinsia, na ustawi wa jamii.
“Mashirika haya yamekuwa mstari wa mbele katika kuleta maendeleo ya watu, na serikali ya awamu ya sita inatambua na kuthamini mchango wao, hasa katika kutoa huduma moja kwa moja kwa jamii,” alisema Mdemu.
Aliongeza kuwa kupitia jukwaa hilo, mashirika yatapata nafasi ya kushiriki moja kwa moja katika kutoa maoni na mapendekezo kwa serikali, hasa kuelekea katika mikakati ya kitaifa kama Dira ya Maendeleo ya Taifa na maandalizi ya uchaguzi mkuu ujao.
Akizungumza kuhusu maandalizi ya kongamano hilo, Msajili wa Mashirika Yasiyo ya Kiserikali, Vickness Mayao, alisema kuwa kongamano hilo ni sehemu ya jukwaa la kitaifa la tathmini ya kazi za mashirika hayo kwa kipindi cha miaka mitano, kwa lengo la kubaini mafanikio, changamoto na maeneo yanayohitaji uboreshaji.
“Ingawa mashirika haya mengi hufanya kazi kwenye mitandao au maeneo ya ndani kwa ndani, kazi zao zimekuwa zikionekana wazi katika jamii. Tunawapongeza kwa kujitoa kwao kuleta mabadiliko,” alisema Vickness Mayao.
Aliongeza kuwa serikali ya awamu ya sita imekuwa na moyo wa ushirikiano na mashirika haya, ikiwemo kuwashirikisha kwenye kutoa maoni katika maandalizi ya Dira ya Maendeleo ya Taifa, jambo linalothibitisha dhamira ya kweli ya ushirikishwaji wa wadau katika maamuzi ya kitaifa.
Kwa upande wake, Mjumbe wa Bodi ya Taifa ya Mtandao wa Mashirika Yasiyo ya Kiserikali (TANGO) na Afisa Mahusiano wa Asasi za Kiraia Mkoa wa Iringa, Charles Lwabulala, alisema TANGO itaendelea kuwaunganisha wanachama kutoka mashirika mbalimbali ili kuangazia mafanikio na mapungufu yanayopatikana katika utekelezaji wa kazi zao.
“Kongamano hili litatoa nafasi kwa mashirika kueleza changamoto zao moja kwa moja mbele ya serikali, ili kuyatafutia majibu ya pamoja kwa ajili ya ustawi wa Taifa,” alisema Lwabulala.
Aidha, mashirika yamehimizwa kutumia jukwaa hilo kutoa elimu kwa jamii kuhusu haki za kiraia na ushiriki katika uchaguzi, ili kuongeza mwamko wa wananchi kushiriki katika kuamua mustakabali wa nchi yao.
Mwisho
0 Comments