Header Ads Widget

COSTECH YAJENGA KITOVU CHA TAASISI ZA UBUNIFU NA UTAFITI DODOMA


Na Hamida Ramadhan, Matukio Daima Media Dodoma

TUME ya Sayansi na Teknolojia Tanzania (COSTECH) inatekeleza kwa kasi mradi wa kimkakati wa ujenzi wa Makao Makuu mapya jijini Dodoma, ikiwa ni hatua ya kuiweka Tanzania kwenye msitari wa mbele katika maendeleo ya maarifa, utafiti na ubunifu wa kisayansi.


Ujenzi huo, unaotarajiwa kukamilika Machi 2026, umeelezewa na viongozi wa COSTECH kuwa ni zaidi ya jengo bali ni uwekezaji wa taifa katika mustakabali wa uchumi wa ubunifu na teknolojia ya kisasa.



Kwa mujibu wa Dkt. Amos Nungu, Mkurugenzi Mkuu wa COSTECH, jengo hilo litakuwa na uwezo wa kutoa huduma kwa watafiti, wabunifu na wajasiriamali wa teknolojia kwa kutumia miundombinu ya kisasa ikiwemo maabara bunifu, vituo vya Atamizi, kumbi za mikutano ya wataalamu, na ofisi zilizounganishwa na mifumo ya kidigitali.


 “Tunajenga jukwaa la kisayansi litakalosaidia taifa kufanya maamuzi yanayotokana na ushahidi, tafiti, na maarifa. Dodoma sasa inapata nafasi ya kuwa moyo wa uvumbuzi nchini,” alisema Dkt. Nungu.


Naye Mwenyekiti wa Bodi ya COSTECH, Prof. John Kondolo, alisema jengo hilo litaimarisha uwezo wa kitaasisi wa COSTECH kusimamia ajenda ya kitaifa ya Sayansi, Teknolojia na Ubunifu (STI), huku likichochea fursa mpya za ajira, ujasiriamali na ushirikiano wa kitaifa na kimataifa.


“Huu ni mwanzo wa awamu mpya ya usimamizi wa tafiti na matumizi ya sayansi kwa maendeleo ya taifa ni jengo lenye dhamira pana ya kizazi kijacho,” alisisitiza Prof. Kondolo.


Masanifu wa jengo hilo, Benedict Martin, amesema usanifu umezingatia uimara wa muda mrefu, tija ya matumizi ya nishati, na uwezo wa kubeba teknolojia za mabadiliko ya kidijitali bila hitaji la maboresho ya haraka.



Kwa mujibu wa COSTECH, jengo hilo ni sehemu ya mpango wa kitaifa wa kuhamasisha matumizi ya teknolojia katika sekta zote na kujenga msingi wa Tanzania kuelekea uchumi wa maarifa na wa kidigitali ifikapo 2030.


Mwisho

Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI