Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Rais wa Umoja wa Mabunge Duniani (IPU), Mhe. Dkt. Tulia Ackson, amewataka vijana wa Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM) kutonyamaza bali kujitokeza kwa ujasiri kuyasema na kuyatangaza mafanikio yanayopatikana chini ya Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Dkt. Tulia amesema kuwa ndani ya kipindi kifupi cha uongozi wa Rais Samia, Serikali imewekeza kwa kiwango kikubwa katika sekta mbalimbali ikiwemo elimu, afya, miundombinu na maendeleo ya vijana, hivyo ni wajibu wa vijana kuyatambua na kuyaeleza mafanikio hayo kwa jamii.
Ameyasema hayo leo tarehe 6 Juni 2025, wakati wa hafla ya mahafali ya Seneti ya Vyuo na Vyuo Vikuu vya Dar es Salaam iliyofanyika katika Ukumbi wa Ubungo Plaza, Wilaya ya Ubungo, jijini Dar es Salaam.
“Ni lazima jamii ifahamu kazi kubwa na nzuri inayofanywa na Serikali yao. Wajibu wenu kama kizazi cha sasa na kizazi cha kesho ni kuwa mstari wa mbele katika kuyasema na kuyaeleza mafanikio haya ili jamii iwe na uelewa wa pamoja kuhusu Serikali ya,” amesisitiza Dkt. Tulia.
Aidha, amewakumbusha vijana kutojidharau wala kukata tamaa, bali wachangamkie fursa zilizopo katika maeneo yao kwa lengo la kujenga taifa imara. Ameongeza kuwa Serikali imefungua milango ya nafasi mbalimbali kwa ajili ya vijana, hivyo ni muhimu kwao kushiriki kikamilifu na kwa ujasiri katika Uchaguzi Mkuu unaotarajiwa kufanyika mwezi Oktoba 2025, kwa kujitokeza kugombea nafasi mbalimbali za uongozi.
0 Comments