Na Hamida Ramadhan, MatuikoDaima App Dodoma
WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu), Mhe. William M. Lukuvi, amesema kuwa jumla ya tani 2,307.37 za bangi zimekamatwa nchini kwa mwaka 2024, ikiwa ni kiwango kikubwa zaidi kuwahi kuripotiwa kwa dawa hiyo ya kulevya.
Akizungumza jijini Dodoma, Waziri Lukuvi alisema kati ya kiasi hicho, tani 2,303.2 ni bangi ya kawaida iliyozalishwa ndani ya nchi, huku tani 4.17 zikiwa ni bangi aina ya Skanka, inayojulikana kwa kuwa na kiwango kikubwa cha kemikali ya THC, iliyoingizwa kutoka baadhi ya nchi za Kusini mwa Afrika.
Kwa mujibu wa Waziri Lukuvi, kiwango cha Skanka kilichokamatwa kimeongezeka kwa asilimia 89.8 ikilinganishwa na mwaka 2023, jambo linaloashiria kuimarika kwa udhibiti na usimamizi wa mipaka, viwanja vya ndege na bandari nchini.
Aliongeza kuwa pamoja na bangi, dawa nyingine za kulevya zilizokamatwa ni mirungi yenye uzito wa tani 18.45, methamphetamine tani 1.7, heroin kilogramu 433.02 na cocaine gramu 853.
Aidha, kwa mara ya kwanza serikali ilikamata kilogramu tano za dawa mpya ya kulevya inayojulikana kama methylene-dioxy-pyrovalerone (MDPV).
Waziri Lukuvi alieleza kuwa mafanikio hayo yametokana na kazi kubwa inayofanywa na vyombo vya ulinzi na usalama kwa kushirikiana na Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya.
Alisema kuwa serikali pia imeimarisha ufuatiliaji wa kemikali bashirifu na dawa tiba zenye asili ya kulevya, ambapo kwa mwaka 2024 zilikamatwa kilogramu 19.2 na lita 22,682.4 za kemikali hizo.
Aidha, serikali kupitia mifumo ya kielektroniki ilizuia uingizwaji wa tani 29.6 na lita 125 za kemikali bashirifu ambazo huweza kutumika kutengeneza dawa haramu.
Katika hatua za kusaidia waraibu wa dawa za kulevya kurejea katika maisha ya kawaida, Waziri Lukuvi alisema serikali iliendelea kutoa tiba ya methadone kupitia vituo 16 vilivyosajili waraibu 17,975 wa dawa jamii ya afyuni, hususan heroin.
Vilevile, nyumba 62 za upataji nafuu (sober houses) ziliendelea kutoa huduma kwa waraibu 17,230 wa dawa mbalimbali.
Waziri Lukuvi alitumia fursa hiyo kumpongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa dhamira yake ya dhati ya kupambana na biashara haramu ya dawa za kulevya na kuwezesha kikamilifu mamlaka na vyombo vya dola katika vita hivyo.
Alisema juhudi hizo zinaendelea kuzaa matunda na kuifanya Tanzania kuwa na mifumo madhubuti ya kudhibiti biashara hiyo haramu.
0 Comments