Na Hamida Ramadhan, MatukioDaima Habari App Dodoma
MKURUGENZI Mtendaji wa shirika lisilo la kiserikali la Foundation for Disabilities Hope (FDH), Maiko Salali, amesema kuwa watu wenye ulemavu nchini wanatembea kifua mbele kutokana na hatua na juhudi madhubuti zinazochukuliwa na Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan katika kuwawezesha kiuchumi na kijamii.
Akizungumza jijini Dodoma, Salali amesema kuwa chini ya uongozi wa Rais Samia, maisha ya watu wenye ulemavu yameanza kubadilika kwa kasi chanya, huku fursa za kiuchumi zikiendelea kufunguka kwa kundi hilo ambalo kwa muda mrefu lilikuwa nyuma katika maendeleo ya taifa.
“Watu wenye ulemavu sasa wanatembea kifua mbele tumekuwa sehemu ya maendeleo ya taifa kwa vitendo, si kwa maneno. Serikali imetupa nafasi na matumaini mapya,” amesema Salali.
Katika hatua hiyo, alitoa shukrani maalum kwa Shirika la Madini la Taifa (STAMICO) kwa kushirikiana na FDH katika kuwawezesha watu wenye ulemavu. Alisema kuwa shirika hilo limekuwa sehemu ya mafanikio yao kwa kuwapatia msaada wa kifedha na vifaa, ukiwemo ufadhili wa kontena la kisasa la kuuzia mkaa katika eneo la Nzuguni jijini Dodoma.
“Shukrani za dhati kwa STAMICO kwa kutupatia kontena la biashara ya mkaa mbadala ambao ni nishati safi Hii si tu fursa ya kipato, bali ni heshima na ishara ya kuwa watu wenye ulemavu si tegemezi tena. Sasa hatuombiomba tena mitaani au barabarani. Tunafanya kazi na kujitegemea,” amesema.
Aidha, Salali alisisitiza kuwa mwaka huu wa uchaguzi, watu wenye ulemavu hawatakuwa kimya. “Mwaka huu ni mwaka wa uchaguzi. Tunatambua mchango wa Rais Samia na hatutaliacha jina lake kwani amefanya mengi kwetu,” amesema
Katika kutambua mchango wa STAMICO, FDH ilikabidhi tuzo ya heshima kwa shirika hilo kwa mchango wake endelevu katika kuboresha maisha ya watu wenye ulemavu na kuonesha mfano wa ushirikiano wa kweli kati ya sekta ya umma na makundi maalum ya kijamii.
Salali alihitimisha kwa kuitaka jamii kuondoa dhana potofu dhidi ya watu wenye ulemavu na kuwatambua kama rasilimali muhimu katika maendeleo ya taifa.
0 Comments