TAMASHA la Kizimkazi linatarajiwa kufanyika Julai 19 hadi 26 mwaka huu katika uwanja wa Suluhu Sport Academy Kizimkazi likiambatana na matukio mbalimbali ikiwemo dua ya kuliombea taifa na wakuu wa nchi.
Akitoa taarifa kwa vyombo vya habari katika hoteli ya kwanza Kizimkazi, Mwenyekiti wa Kamati ya Kizimkazi, Mahfoudh Said Omar alisema, mwaka huu Tamasha hilo litakuwa la aina yake lengo ni kuitangaza Kusini kiutalii kupitia vivutio vyake vilivyopo ikiwemo rasilimali ya bahari, utamaduni na sanaa.
Aidha alisema tamasha hilo litaangazia kwa kina utajiri wa rasilimali ya bahari, utamaduni wa kipekee wa wakazi wa Kusini na sanaa mbalimbali zinazotambulisha utambulisho wa eneo hilo.
"Lengo letu ni kuonyesha uzuri wa Kusini na kuwavutia watalii wa ndani na nje ya nchi kutembelea maeneo haya ambayo yamejaa utajiri mkubwa wa vivutio vya kiasili na kitamaduni," alisema.
Akizungumzia mafanikio yatakayopatikana kwa wananchi wa kizimkazi, alisema ni uwepo wa fursa mbalimbali hasa za kibiashara kwa wajasiriamali, wavuvi, wafugaji kuuza bidhaa zao na hata kuongeza uchumi wa nchi.
“Wananchi wataweza kuuza bidhaa zao mbalimbali, wakiwemo wavuvi, wafugaji, wakulima na wajasiriamali hii ni fursa kubwa ya kiuchumi itakayowawezesha kuongeza kipato chao na kuchangia pato la taifa kupitia sekta ya utalii,” alisema.
Aidha, alibainisha kuwa tamasha hilo litaendelea kuwa chachu ya maendeleo ya kijamii na kiutamaduni, kwa kuhamasisha ushiriki wa vijana, vikundi vya sanaa huku likitangaza vivutio vya kipekee vilivyopo Kusini mwa Tanzania.
Mwenyekiti Mahfoud alibainisha kuwa tamasha hilo litafunguliwa rasmi na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Hussein Ali Mwinyi Julai 19 mwaka huu.
Naye Katibu wa Tamasha hilo Hamid Abdul- hamid Khamis alisema tamasha hilo litaanza kwa mafunzo maalum kwa sekta saba ikiwemo wavuvi, wafugaji, utalii na wajasiriamali.
Alisema mafunzo hayo yataanza Julai 12 na yatafungwa rasmi na Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Dk Samia Suluhu Hassan Julai 20.
Aidha alisema Julai 16 kutakuwa na dua ya kuwaombea viongozi wakuu wa nchi Dk.Samia na Dk. Mwinyi ambayo itafanyika katika viwanja vya Mnazimmoja na dua nyengine ya kuwaombea wakuu wa nchi na wazee waliotangulia mbele ya haki itakayofanyika Julai 18 katika msikiti wa Kizimkazi Dimbani.
Hata hivyo alisema siku hiyo hiyo kutakuwa na kongamano la nishati asilia ambalo lirafanyika katika hoteli ya Kwanza Kizimkazi ambalo litatoa fursa juu ya matumizi sahihi ya nishati ya kupikia.
Katibu huyo alisema matukio mengine ni upimaji wa afya, mashindano ya kuhifadhi kuraan yatakayofanyika katika skuli ya sekondari Hasnuu Makame na ufunguzi wa kiwanja cha kufurahishia watoto Julai 24 katika eneo la Kibuteni na baadae kutembelea mabanda ya maonesho ya biashara katika viwanja vya Suluhu Sports Academy.
Hata hivyo alisema Julai 25 Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Dk.Samia Sulubu Hassan atafungua skuli ya sekondari Makunduchi na baadae kuzindua hoteli ya Johari.
Sambamba na hayo Dk. Samia Suluhu Hassan anararajiwa kuwa mgeni rasmi katika kilele cha tamasha hilo Juali 26
Mmoja wa wasisi wa Tamasha hilo, Said Hamad Ramadhan, alisema tamasha hilo lina manufaa na kichocheo kikubwa cha maendeleo kwa wilaya hiyo na Zanzibar kwa ujumla.
Tamasha hilo linatarajiwa kuwashirikisha wadau mbalimbali wa utalii, wasanii, wanamichezo na vikundi vya utamaduni, likiwa ni jukwaa la kuhamasisha utalii na kuinua uchumi wa jamii za ukanda huo kupitia sekta ya burudani na utalii endelevu linalokwenda sambamba na kauli mbiu ya mwaka huu isemayo Kizimkazi Kumenoga.
0 Comments