Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira Same–Mwanga (SAMWASA) imeanza kutekeleza programu maalum inayojulikana kama ZUMA – kifupi cha Zuia Upotevu wa Maji, ambayo inalenga kuboresha huduma kwa wateja na kupambana na changamoto ya wizi wa maji, upotevu wa mapato pamoja na dosari za kiufundi kwenye miundombinu.
Hayo yameelezwa na Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira Same-Mwanga (SAMWASA), Mhandisi Rashid Shaban, amesema programu hiyo inahusisha operesheni ya kuzunguka nyumba kwa nyumba katika maeneo mbalimbali ya mamlaka hiyo kwa lengo la kubaini hali halisi ya upatikanaji wa huduma, mifumo ya uunganishaji wa maji, usahihi wa taarifa za wateja, miundombinu ya mamlaka na kuweka mkazo katika kudhibiti matumizi haramu ya maji.
“Tumeanza utekelezaji wa programu hii Jumatano ya mwisho wa mwezi Mei, 2025, na tutaifanya mara mbili kila mwezi. Tayari katika siku ya kwanza ya utekelezaji tumebaini mambo mengi yanayohitaji ufuatiliaji wa karibu, ikiwa ni pamoja na watumishi wasio waadilifu kushirikiana na baadhi ya wateja kutumia maji kinyume na utaratibu, wizi wa maji kupitia miunganisho isiyo rasmi, pamoja na changamoto ya miundombinu inayosababisha mivujo na upotevu wa maji,” alisema Mhandisi Rashid.
Amesema kuwa wateja wengine wamebainika kutumia huduma ya maji bila kuwa na mita, hali inayosababisha mamlaka kushindwa kupata mapato stahiki.
“Kuna baadhi ya maeneo wateja wanatumia maji bila mita wala mkataba halali. Hii ni moja ya sababu zinazochangia upotevu mkubwa wa mapato na inakwamisha jitihada za mamlaka kuboresha huduma na kupanua mtandao wa usambazaji maji,” ameongeza.
Mhandisi Rashid ameonya kuwa hatua kali zitachukuliwa dhidi ya watumishi wa mamlaka watakaobainika kushiriki kwenye vitendo vya ukwepaji wa taratibu au kushirikiana na wateja kuunganisha maji kwa njia za udanganyifu. Vilevile, ametoa wito kwa wananchi kushirikiana na mamlaka hiyo kwa kutoa taarifa sahihi, kulipa Ankara kwa wakati, na kuhakikisha taarifa zao zimesajiliwa kwenye mfumo rasmi wa mamlaka.
Kwa mujibu wa sheria za maji, kuunganisha maji kwa njia ya wizi au udanganyifu ni kosa la jinai linalostahili adhabu, ikiwemo faini au hatua nyingine za kisheria. Mamlaka imeeleza kuwa haitamvumilia yeyote atakayebainika kuvunja sheria hizo.
Baadhi ya watumishi wa SAMWASA waliokuwa kwenye operesheni hiyo wameeleza kuwa katika maeneo mbalimbali walikokagua, ikiwemo vituo vya mafuta, nyumba za kulala wageni, makazi ya watu na maeneo ya biashara, walibaini uwepo wa miunganisho ya maji isiyo na mita, mivujo, madeni makubwa, na baadhi ya wateja kutumia deni kama kisingizio cha kutolipa Ankara kwa wakati.
Programu ya ZUMA inalenga si tu kudhibiti matumizi haramu ya maji, bali pia kusaidia mamlaka kuongeza mapato, kujenga uaminifu kwa wateja, kuboresha miundombinu na hatimaye kusogeza huduma bora kwa wananchi katika maeneo yote yanayohudumiwa na SAMWASA.
0 Comments