Header Ads Widget

RAIS SAMIA MGENI RASMI GRAND BUNGE BONANZA DODOMA

Na Hamida Ramadhan,Matukio Daima App Dodoma

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika Bonanza la Bunge, linalotarajiwa kufanyika Juni 21, 2025 kwenye viwanja vya Shule ya Sekondari John Merin, Miyuji jijini Dodoma.

Bonanza hilo ambalo limepewa kaulimbiu “Shiriki Uchaguzi Mkuu kwa Maendeleo ya Taifa,” linaandaliwa kwa kushirikiana na Benki ya CRDB, na linalenga kuhamasisha wananchi kushiriki kikamilifu katika Uchaguzi Mkuu unaotarajiwa kufanyika baadaye mwaka huu.

Akizungumza kuhusu maandalizi hayo, Mwenyekiti wa Bonanza la Bunge, Mheshimiwa Festo Sanga, alisema kuwa Bonanza hilo ni sehemu ya kuhitimisha shughuli za Bunge kwa kipindi cha miaka mitano, na pia kuwaunganisha wabunge, wananchi na wadau kupitia michezo na burudani zenye ujumbe wa amani, mshikamano na demokrasia.

“Bonanza la mwaka huu ni kubwa na la kipekee kwa sababu linahitimisha kipindi cha Bunge na linafungua ukurasa mpya kuelekea uchaguzi. Tunamshukuru Rais kwa kukubali kuwa mgeni rasmi na kuwa sehemu ya kuhamasisha ushiriki wa wananchi kwenye mchakato wa uchaguzi,” alisema Sanga.

Katika bonanza hilo, michezo mbalimbali itafanyika ikiwemo mpira wa miguu, pete, kikapu, mpira wa wavu na kuvuta kamba. Pia kutakuwa na matembezi ya hiari yatakayoanzia Chuo cha Mipango hadi viwanja vya bonanza ikiwa ni sehemu ya kuhamasisha mazoezi na afya bora.

Benki ya CRDB ambayo ni mdhamini mkuu wa bonanza hilo, imetoa msaada wa vifaa vya michezo vyenye thamani ya zaidi ya shilingi milioni 130. Mwakilishi wa benki hiyo, Ntully Mwambapa, alisema kuwa CRDB itaendelea kushirikiana na Bunge kuandaa matukio ya kijamii na kimaendeleo yanayolenga afya, mshikamano na ustawi wa wananchi.


“Tunatambua nafasi ya michezo katika kuleta watu pamoja. Bonanza hili pia ni sehemu ya kuwapongeza wabunge kwa utumishi wao wa miaka mitano. Tunatoa wito kwa wananchi wote wa Dodoma kushiriki,” alisema Ntully.

Sanga aliongeza kuwa taasisi nyingine za umma na binafsi zinaalikwa kuiga mfano wa CRDB kwa kushiriki katika mabonanza mbalimbali, akisisitiza kuwa michezo ni daraja la amani na maendeleo. Bonanza hilo litakuwa na burudani mbalimbali, huduma kwa jamii na nafasi kwa wananchi kuonana moja kwa moja na viongozi wao.

Bonanza la Bunge la mwaka 2025 linatarajiwa kuwa tukio la kihistoria, likiwaunganisha Watanzania kuelekea Uchaguzi Mkuu kwa njia ya michezo, afya na uzalendo.

Mwisho

Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI