Na Hamida Ramadhan,Matukio Daima App Dodoma
KATIKA kuadhimisha Wiki ya Utumishi wa Umma mwaka 2025, Taasisi ya Mifupa Muhimbili (MOI) imesema imewahudumia zaidi ya wagonjwa 70 katika banda lao lililopo kwenye Viwanja vya Chinangali Park jijini Dodoma, huku huduma nyingi zikitolewa kwa wagonjwa wa mifupa, ubongo na mishipa ya fahamu.
Akizungumza na waandishi wa habari, Dkt. Tumaini Minja Dakitari bingwa wa upasuaji mifupa Moi , alisema kuwa wagonjwa wengi waliowahudumia ni wenye matatizo ya maumivu sugu ya mgongo, magoti, nyonga na mishipa ya fahamu kwa ujumla, ambapo baadhi ni wagonjwa waliowahi kutibiwa MOI na wengine ni wapya waliopata huduma kwa mara ya kwanza wwngine wenyeji wa Dodoma na wanaotokea pembezoni .
“Wagonjwa wengi wanaotufikia ni wa umri kati ya miaka 45 hadi 60, na matatizo yao yanatokana zaidi na changamoto za umri, uzito mkubwa kupita kiasi, pamoja na mitindo ya maisha isiyojumuisha mazoezi ya mwili,” alisema Dkt. Minja.
Aliongeza kuwa magonjwa hayo yanatibika kulingana na hali ya mgonjwa, ambapo wengine huhitaji upasuaji na wengine hutibiwa kwa kutumia dawa au njia mbadala zisizo za upasuaji. Dkt. Minja alisema huduma wanazotoa kwenye maonesho hayo ni pamoja na uchunguzi wa awali, ushauri wa kitabibu na upangaji wa rufaa kwa matibabu zaidi MOI.
Aidha, MOI imejipanga kutoa huduma mahsusi kwa wanamichezo, kwani wengi wao hukumbwa na majeraha ya magoti, enka na viungo mbalimbali kutokana na shughuli zao.
Alisema kuwa changamoto kubwa kwa wanamichezo wengi ni kutofuata ushauri wa kitaalamu na kuchelewa kufika hospitali hadi hali inapoendelea kuwa mbaya.
“Tunawahamasisha wanamichezo wote kutembelea banda letu hapa Chinangali kwa ajili ya uchunguzi wa awali na kupata ushauri wa kiafya kabla ya majeraha kuwa makubwa. Matibabu si lazima yaanze baada ya maumivu, kinga ni bora zaidi,” alisisitiza.
Dkt. Minja alihitimisha kwa kuwakaribisha wakazi wa Dodoma na wageni wengine kutembelea banda la MOI ili kupata huduma na elimu kuhusu afya ya mifupa, ubongo na mishipa ya fahamu, akibainisha kuwa taasisi hiyo itaendelea kushiriki kikamilifu katika kuimarisha huduma za afya nchini.
Mwisho
0 Comments