Na Ashrack Miraji, Matukio Daima
Mwenge wa Uhuru umeingia rasmi katika Halmashauri ya Wilaya ya Lushoto leo, baada ya kukabidhiwa kutoka Halmashauri ya Bumbuli, ambapo utakimbizwa umbali wa kilomita 112.8 kupitia tarafa mbili, kata nne na vijiji 23. Katika mbio hizo, Mwenge utakagua na kuzindua miradi ya maendeleo yenye thamani ya zaidi ya shilingi bilioni 1.8.
Akizungumza mara baada ya makabidhiano hayo, Mkuu wa Wilaya ya Lushoto, Zephania Sumaye, alisema kuwa kaulimbiu ya Mwenge wa mwaka huu ni: “Jitokeze Kushiriki Uchaguzi Mkuu 2025 kwa Amani na Utulivu,” ambayo inaakisi dhamira ya kitaifa ya kuhamasisha ushiriki wa wananchi katika mchakato wa kidemokrasia kwa njia ya amani na utulivu.
“Tumepokea Mwenge wa Uhuru tukiwa na maandalizi kamili. Kauli mbiu ya mwaka huu ni wito kwa kila Mtanzania kushiriki uchaguzi mkuu ujao kwa njia ya amani, busara na utulivu,” alisema Sumaye.
Aliongeza kuwa Mwenge huo utakagua na kuzindua miradi saba ya maendeleo inayogusa sekta mbalimbali kama elimu, afya, maji na miundombinu, ikiwa ni ishara ya dhamira ya Serikali katika kuwahudumia wananchi, hasa wa maeneo ya vijijini.
“Kwa jumla, miradi tunayokwenda kukagua ina thamani ya shilingi bilioni 1.8. Hii inaonesha jitihada kubwa zinazofanywa kuhakikisha maendeleo yanawafikia wananchi wote,” aliongeza Mkuu huyo wa Wilaya.
Sumaye pia alitoa wito kwa wananchi kujitokeza kwa wingi katika mapokezi ya Mwenge huo, sambamba na kudumisha mshikamano na amani kuelekea uchaguzi mkuu wa mwaka 2025.
Mwenge wa Uhuru ni alama ya mshikamano wa kitaifa na maendeleo, ambao huzunguka nchini kote kila mwaka tangu mwaka 1961 kwa lengo la kuhamasisha maendeleo, uwajibikaji wa kijamii, mshikamano wa kitaifa, na sasa zaidi — ushiriki wa amani katika chaguzi za kidemokrasia.
0 Comments