Header Ads Widget

MBUNGE NJEZA AWATETEA WAKULIMA WA PARETO BUNGENI KISA BEI DUNI

 

Mbunge wa jimbo la Mbeya vijijini Mhe. Oran Njeza, ameihoji Serikali juu ya mkakati wake wa kuongeza uzalishaji wa zao la Pareto ikiwa ni pamoja na kuboresha soko la uhakika la zao hilo ili kumnufaisha mkulima tofauti na sasa ambapo anasema mnunuzi wa kati na wa mwisho ndio wanufaika wakubwa.

Akijibu swali la msingi la Mbunge wa Mbeya vijijini Oran Njeza bungeni jijini Dodoma, Naibu Waziri wa Kilimo Mhe. David Ernest Silinde amesema ni mkakati wa Serikali kuboresha sekta ya kilimo ambapo Serikali ya awamu ya sita imetilia maanani pia mazao ambayo hapo awali yalikuwa hayapewi kipaumbele ikiwemo Pareto.


Amesema Serikali imepanga kwa mwaka wa fedha 2025/2026 kuongeza thamani ya zao hilo ikiwemo kusambaza mbegu bora kwa wakulima kwenye maeneo yanayolima zao hilo ikiwemo Manyara, Mbeya na Songwe.

Katika swali lake la nyongeza Mbunge Oran Njeza amehoji

"Mhe. Mwenyekiti kuna changamoto kubwa sana ya mnyororo wa thamani ya hili zao (Pareto), mkulima analipwa shs. 3,700 kwa kilo wakati mnunuzi akiisaga analipwa shilingi 6000 kwa kilo na ikichunjwa inauzwa laki mbili na mwishowe bei ya Dunia ni shilingi 1,000,000 (Tsh. Million moja) kwa kilo ya Pareto na ukiangalia mkakati uliopo sio mzuri na haumsaidii mkulima wala nchi yetu sasa kwanini bodi ya Pareto isirudishwe ili kuokoa uzalishaji wa zao hili muhimu!", amehoji Mbunge wa jimbo la Mbeya vijijini.

Pamoja na hayo Mhe. Njeza ameishauri Serikali kutumia kiwanda cha viuadudu TBPL kilichopo katika eneo la Kibaha mkoani Pwani ili kuanza kuzalisha viatilifu ndani ya nchi hatua itakayosaidia kupunguza gharama na bei za viatilifu na kukuza uzalishaji wa zao hilo kwa wakulima.

Akijibu swali hilo Naibu Waziri Silinde, amesema Serikali inazingatia maoni yake na ndio maana imeendelea kuboresha sekta ya kilimo kwa kufufua na kuyapa kipaumbele mazao ambayo haya kuwa na thamani hapo awali na kuhusu bodi ya Pareto amesema kwa sasa inaendelea kusimamiwa na bodi ya mazao mchanganyiko na Wizara ya Kilimo itaendelea kuliangalia kulingana na uzalishaji wa zao hilo utakavyoendelea.

Kuhusu kufufua kiwanda cha viatilifu Naibu Waziri wa Kilimo amesema pia suala hilo lipo kwenye mipango ya Serikali hivyo kumwondoa shaka Mbunge Njeza na wananchi kwa ujumla hasa wanaohusika kwa namna moja ama nyingine na zao la Pareto katika maeneo mbalimbali hapa nchini.

Tanzania inaongoza kwa zao la Pareto katika bara la Africa ambapo kwa Tanzania zao hilo linalimwa katika maeneo mbalimbali ikiwemo Halmashauri za Mbeya, Ileje (Songwe), Ludewa (Njombe), Mbulu (Manyara), Makete (Njombe) na Arusha huku Pareto bora kwa Tanzania ikitajwa kutoka Mbeya vijijini ambapo pamoja na ubora wa Pareto ya Tanzania bado bei yake ni ndogo ikilinganishwa na ile ya soko la Dunia hasa kwa mnunuzi wa mwisho hivyo ni vema Serikali ikatilia maanani kuhakikisha zao hili pia linaleta tija zaidi hasa kwa mkulima kupitia mipango inayoelezwa na Serikali ya Tanzania katika kuboresha zao hilo ikiwemo kuongeza uzalishaji wa mbegu na kutoa elimu ya kilimo bora cha Pareto kwa wakulima.

Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI