WAZIRI wa Fedha, Dkt. Mwigulu Nchemba, amesema kuwa Serikali imefanikiwa kuimarisha hali ya uchumi wa nchi kwa mwaka 2024 baada ya kufikia ukuaji wa Pato la Taifa kwa asilimia 5.4.
Akizungumza leo bungeni jijini Dodoma wakati akiwasilisha bajeti ya Wizara ya Fedha kwa mwaka 2025/2026, Waziri Mwigulu alisema Serikali iliweka malengo ya kujenga uchumi jumuishi, endelevu na unaohimili misukosuko ya kiuchumi duniani.
Amesema katika mwaka 2024, Serikali ilitarajia kuona uchumi wa Taifa ukikua kwa asilimia 5.4 kutoka asilimia 5.1 mwaka 2023.
Aidha, mfumuko wa bei ulipangwa kubaki katika wastani wa asilimia 3.0 hadi 5.0 huku mapato ya ndani yakitarajiwa kufikia asilimia 15.8 ya Pato la Taifa. Mapato ya kodi yalilenga kufikia asilimia 12.9, na nakisi ya bajeti (pamoja na misaada) kutozidi asilimia 3.0 ya Pato la Taifa.
Waziri Nchemba amesema kuwa akiba ya fedha za kigeni ilitarajiwa kuwa ya kutosha kugharamia uagizaji wa bidhaa na huduma kutoka nje kwa angalau miezi minne, jambo ambalo limefanikiwa kufikiwa hadi Machi 2025, ambapo akiba hiyo ilifikia dola za Marekani milioni 5,693.2.
Amesema mafanikio hayo yametokana na utekelezaji wa sera madhubuti za kiuchumi, zikiwemo kudhibiti mfumuko wa bei, kuhudumia deni la Serikali kwa wakati, kuelekeza fedha kwenye miradi yenye tija kwa uchumi, kuboresha mazingira ya biashara na uwekezaji pamoja na kuongeza mauzo ya bidhaa na huduma nje ya nchi.
Katika kipindi cha Julai 2024 hadi Aprili 2025, mfumuko wa bei nchini ulipungua hadi wastani wa asilimia 3.1 ikilinganishwa na asilimia 3.2 katika kipindi kama hicho mwaka 2023. Waziri amesema kuwa hali hiyo imetokana na usimamizi madhubuti wa sera za fedha na bajeti.
Kuhusu utekelezaji wa bajeti ya Serikali, Dkt. Mwigulu amesema kuwa wizara imefanikiwa kuandaa miongozo ya kisera, kisheria na kitaalamu, ikiwemo Mwongozo wa Maandalizi ya Mpango na Bajeti ya Serikali kwa mwaka wa fedha 2025/2026.
Kwa upande wa matumizi, amesema jumla ya Shilingi trilioni 38.10 zilitolewa, ambapo Shilingi trilioni 25.14 zilitumika kwa matumizi ya kawaida na Shilingi trilioni 12.96 kwa matumizi ya maendeleo.
Waziri ameongeza kuwa kati ya fedha hizo, Shilingi bilioni 996.5 zilitolewa kwa ajili ya malipo ya wakandarasi, wazabuni na watumishi wa umma. Kati ya kiasi hicho, wakandarasi walilipwa Shilingi bilioni 918.8, wazabuni Shilingi bilioni 38.4, na watumishi wa umma walipokea Shilingi bilioni 38.8.
Kwa mujibu wa Waziri, mafanikio haya ni uthibitisho wa uimara wa uchumi wa Taifa na uwezo wa Serikali kusimamia rasilimali za umma kwa ufanisi katika mazingira yenye changamoto nyingi za kimataifa.
0 Comments