Mkuu wa wilaya ya Mbeya Mhe. Beno Malisa kwa niaba ya mkuu wa mkoa wa Mbeya Mhe. Dkt. Juma Homera, amefika katika eneo la Iwambi kwa ajili ya kujionea ujenzi wa barabara ya mchepuko kutoka Iwambi hadi Mbalizi kama ilivyoelekezwa na Serikali kuu kuona miundombinu hiyo inaboreshwa.
Serikali ya mkoa wa Mbeya kupitia wakala wa barabara Tanzania TANROADS, tayari imeanza kutekeleza agizo hilo lililotolewa na Rais wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan la kutengeneza barabara ya mchepuko katika eneo la Iwambi jijini Mbeya kuunganisha na Mbalizi ili kupunguza madhara yatokanayo na ajali za barabarani.
Ujenzi huo umeanza kutekelezwa na Wakala wa barabara Tanzania TANROADS mkoa wa Mbeya ambapo akizungumza kwenye eneo unakofanyika utengezaji wa barabara hiyo katika kata ya Iwambi, Mkuu wa wilaya ya Mbeya Mhe. Beno Malisa, amesema tayari agizo hilo limeanza kufanyiwa kazi TANROADS mkoa wa Mbeya.
Meneja wa wakala wa barabara Tanzania (TANROADS) mkoa wa Mbeya Mhandisi Masige Matari, amesema tayari wameshafikisha vitendea kazi mbalimbali katika eneo la mradi na kuanza mara moja ujenzi barabara hiyo ikiwa ni pamoja na kuongeza upana wa barabara kuwa mkubwa zaidi ili kumudu magari makubwa kupishana.
Itakumbukwa mnamo Juni 07, 2025 huko katika eneo la Mbalizi mkoani Mbeya ilitokea ajali iliyosababisha umauti wa wananchi 28 na wengine tisa kujeruhiwa, ajali iliyohusisha magari matatu ambayo ni lori aina ya Scania lenye namba za usajili T. 830 EDP lenye tela namba T. 148 CTD, Coaster aina ya Mitsubishi Rosa lenye namba za usajili T. 257 DVP na gari lingine aina ya Toyota Lite Hiace lenye namba za usajili T. 185 DMF baada ya wa dereva wa lori aina ya Scania lenye namba za usajili T. 830 EDP lenye tela namba T. 148 CTD kuendesha gari kwa mwendokasi na kushindwa kulimudu gari lake hilo na hivyo kuyagonga magari mengine mawili.
0 Comments