Header Ads Widget

JE, NO REFORMS NO ELECTION VS OKTOBA TUNATIKI KUZAA MWELEKEO MPYA WA SIASA TANZANIA?

Kwa siku kadhaa sasa kuna sauti mbili zinazoshindana katika mdundo wa ngoma mbili tofauti lakini kwenye uwanja mmoja. Sauti moja inasema No Reform No Election, ikisisitiza mageuzi ya msingi kwanza kufanyika kabla ya uchaguzi. Sauti nyingine ikiitika; Oktoba Tunatiki, kauli ya ujasiri wa kusonga mbele, hata bila dhamana ya mabadiliko kamili.

Huu si ubishi wa kawaida. Ni mgongano wa falsafa, mtazamo na matarajio. Ni sauti ya kizazi kipya kinachotafuta nafasi ya kusema, kuamua, na kudai hata kama ni kwa kupitia ujumbe wenye maneno mawili au matano.

Katika nchi ambayo historia ya uchaguzi wake imejaa mchanganyiko wa changamoto na matumaini kutokana na uchanga wake kwenye demokrasia, sasa tunashuhudia aina mpya ya siasa na harakati. Siana na harakati zisizo na silaha, bali hashtags, ujumbe, picha, sauti na video. Harakati zisizo na maandamano wala matusi, bali machapisho mitandaoni.

Lakini je, huu mgongano huu unaisha kwenye mitandao au unatafsiriwa katika uhalisia wa siasa ya Tanzania?

KINACHOENDELEA MITANDAONI TANZANIA


Moja ya picha bango zinazosambazwa kwenye mitandao kutoka upande wa wanaopigia debe 'No Reforms No election'

Katika karibu Juma moja sasa, maneno sita yamekuwa maarufu zaidi na yakitajwa na kutumika sana mitandaoni yanahusisha kampeni na harakati za pande mbili kuhusu Uchaguzi mkuu wa Tanzania wa Oktoba mwaka huu

Kampeni ya No Reforms No Election, inayoongozwa na chama kikuu cha upinzani, Chadema na wanaharakati wa mageuzi, imejikita kwenye matumizi ya nguvu ya kidijitali, kuanzia hashtags hadi "comment sections" za viongozi na watu maarufu.

Kila unapofungua kurasa za akaunti za watu maarufu wakiwemo wasanii, viongozi, taasisi za umma na zingine, zimekuwa 'zikishambuliwa' na ujumbe na picha za 'No Reforms No Election'. Kwa siku mbili mfululizo kampeni hii iliteka mitandao karibu yote hasa instagram, mtandao wa X (zamani tweeter) na baadaye Tiktok na kiasi Youtube bila kupata majibu.

Lakini siku zilizofuata kampeni ya Oktoba Tunatiki haikukaa kimya. Imezaliwa kama jibu, sauti ya wale wanaoamini kuwa mabadiliko yanapatikana kwa kushiriki uchaguzi, na si kwa kugomea. Chama tawala cha Mapinduzi (CCM) kinaamini hilo pamoja na vyama vingine, kikiwemo Chaumma, chama kilichoibuka kwa kasi baada ya waliokuwa viongozi kadhaa wa Chadema kuhamia huko wakipinga 'No Reform No election.

Kwa upande wa kampeni ya Oktoba Tunatiki, kumekuwa na picha kadhaa kama hizi zikihamasisha watu kushiriki uchaguzi

Japo kwenye mikutano na hadhira zingine kampeni hizi mbili zinapigwa, lakini kasi yake kwenye mitandao imekuwa kubwa, isivyotarajiwa na ya kushangaza.

Hata wasanii wa kimataifa wameanza kuuliza. Msanii kutoka Nigeria, Chella Boy, aliyekua Tanzania kwa tamasha, alishtushwa na maelfu ya ujumbe aliopokea:

"Nimeogopa, nini hii No Reform No Election? Nimekuwa naiona kila sehemu. Sielewi".

Msanii wa Kuchekesha wa Tanzania, Hakika Rubeni ambaye amekiri kupoteza wafuasi 40,000 ndani ya siku mbili kupitia kampeni ya No Reform No Election, anaduwazwa na kampeni hizi za mtandao zilivyoshika kasi.

Kwa upande wa Serikali haishtushwi sana na hilo ikisema watanzania wana uhuru wa kuongea kwa mujibu wa sheria. Msemaji wa serikali ya Tanzania, Gerson Msigwa, akizungumza na Mwananchi Communications, alisema: "Kinachoendelea kwenye mitandao ni upuuzi. Huwezi kuendesha kampeni ya kuzuia uchaguzi wakati nchi imejiwekea kalenda yake."

"Msipuuze mitandao ya kijamii, ina nguvu kupita kawaida"

Kwa nyakati za sasa si lazima uwe na redio au runinga ili kusikika, wafuasi 'followers' elfu kumi tu wanaweza kuwa bunge lako la mitandaoni. Ukahutubia na wakakusikiliza, ama ukakosolewa na ujumbe ukakufikia.

Nguvu ya mitandao inajionyesha wazi kupitia mazuri yake na mabaya yake. Watumiaji wengi ambao ni vijana, wanatumia mitandao ya kijamii, kufikisha ujumbe kwa haraka na uhamasishaji wa haraka kwa walengwa. Japo kusambaa kwa taarifa za uongo na zinazopotosha kunaiweka mitandao kwenye kona nyingine, nguvu yake huwezi kuipuuza.

"Msipuuze mitandao ya kijamii, ina nguvu kupita kawaida'", kauli ya Aliywahi kuwa Naibu Waziri wa zamani wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo nchini Tanzania, Juliana Shonza alipozungumza na maafisa habari wa serikali miaka mitano iliyopita.

Kinachotokea sasa Tanzania, mitandao kuwa majukwaa ya vuguvugu na Kampeni, kilishatokea na kubadili mwelekeo wa siasa kwa nchi na maeneo mengine duniani.

Kampeni za uchaguzi wa mwaka 2016 nchini Ufilipino, mgombea urais Rodrigo Duterte, ilitumia vikundi vya mitandaoni na akaunti feki kusambaza ujumbe wake, kushambulia wapinzani, na kujijenga kama kiongozi. Walitumia sana Facebook na mitandao mingine kuwafikia wapiga kura moja kwa moja, hatimaye alishinda na kuwa rais wa 16 wa taifa hilo.

Katika vuguvugu la Arab Spring kati ya mwaka 2010-2012, nchi kama Tunisia, Misri, na Libya, mitandao ya kijamii ilitumika kama zana muhimu ya kuhamasisha maandamano, kuratibu harakati, na kusambaza habari kwa kasi kubwa, hasa wakati vyombo vya habari vya serikali vilikuwa vikizuia taarifa.

#EndSARS zilikuwa harakati za maandamano dhidi ya ukatili wa polisi uliotikisa miji mikubwa kusini mwa Nigeria, mitandao ilifanya kazi kubwa kwenye kampeni hii mwaka 2020 kama ilivyofanyika Marekani kupitia Black Lives Matters' kupinga ukatili wa Polisi. Ilianza mwaka 2013 ikasambaa na ikaendelea kutumika kila mtu mweusi anaposhambuliwa ama kuuawa na Polisi. Ikatumika kwenye Kampeni za uchaguzi hasa wakati Barack Obama, Rais wa 44 wa taifa hilo alipokuwa anawania kuingia Ikulu, na imekua ikitumiaka mpaka leo.

Kwenye maandamano ya Kenya mwaka 2024 kupinga muswada wa fedha, mitandao ya kijamii, ilibadili upepo kwa kiasi kikubwa. Mitandao ina nguvu bila shaka.

Siasa za 'hashtag', siasa mpya zitakazoua siasa za majukwaani?

Makamu Mwenyekiti wa CHADEMA Bara, John Heche akichangisha fedha kwenye moja ya majukwaa ya kisiasa yaliyoendesha kampeni ya No Reforms No Election.

Tangu Tanzania izaliwe, eneo kubwa la kupima ushawishi wa chama cha siasa kama kinakubalika ama la ni idadi kubwa ya watu wanaohudhuria kwenye mikutano ya kampeni

Kwa mfano uchaguzi wa mwaka 2015, uliomuweka madarakani hayati John Pombe Magufuli, ulitawaliwa na kampeni ya 'mafuriko', hasa kupitia mgombe wa upinzani, Edward Lowassa, Waziri Mkuu wa zamani ambapo kujaza watu kwenye mikutano ilikua namna pekee ya kuonyesha nguvu yako.

Imekuwa hivyo kwenye chaguzi karibu zote, lakini sasa kidokidogo mitandao inaanza kuchukua nafasi.

"Sasa hivi mitandao imebadilisha sana hulka ya kwa nini mtu anapost (chapisha)", Mkurugenzi wa Shirika la Tech & Media Convergency, Bi. Asha Abinallah anaiambia DW.

Miaka 6 ya kuzuiwa kufanya mikutano ya kisiasa kwa vyama vya siasa, wakati wa utawala wa Magufuli, kumechagiza zaidi matumizi ya miotandao. Mitandao ilionekana ndiyo jukwaa pekee la kupumulia vyama vya siasa, na kupenyeza hoja zao kwa hashtag na ujumbe wa kawaida.

Vyama havikufa, uwepo wao ulionekana kupitia mitandao ya X, Instagram, Tiktok na You tube na Threads. Na sasa ni kama imekuwa njia mujarabu kwao, ambapo kampeni kinzani za No Reforms No Election na ile ya Oktoba Tunatiki zinadhihirisha hilo.

Katibu wa Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa CCM, Amos Makalla anasema No Reform No Election ni nadharia tu za kujifurahisha".

Ingawa hakuna anayejua matokeo halisi ya Kampeni hiyo, kuwepo kwakwe kunatoa sura nyingine ya jukwaa la kufikisha ujumbe kwa haraka na wingi, huku Chama tawala, CCM kinachoongoza serikali kikiendelea kusisitiza kuwa kampeni ya No Reforms No Election ni ya kujifurahisha, haitabadilisha chochote kuhusu Uchaguzi mkuu.

"Hata ungepost (chapisha) posti mamilioni na mamilioni...No Reform No Election, uchaguzi upo pale pale. Haisaidii… ni nadharia tu za kujifurahisha", anasema Amos Makalla, Katibu wa Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa CCM.

Mtazamo wa watumiaji na watalaamu wa masuala ya mitandao wanaonya kwamba mitandao inanafasi kubwa ya kuwa majukwaa mbadala ya mikutano ya kisiasa iliyozoeleka.

"Nchi nyingi zinatumia mitandao kwenye shughuli nyingi ukiacha biashara, burudani, na taarifa za kawaida, hata siasa na kampeni mbalimbali, mitandao imekuwa msaada", na ndiyo maana baadhi ya nchi hasa Afrika, nyakati za Uchaguzi hufungia mitandao kuhofia nguvu zake", anasema Rahman John, Mwalimu na mtaalam wa masuala ya Tehama.

Kwa kauli hii, na huku ikisalia miezi minne kuelekea uchaguzi Mkuu wa Oktoba, kinachoendelea sasa kinaweza kuonekana upepo lakini kinaweza kujenga msingi wa namna kampeni za uchaguzi na siasa zijazo zitakavyoendeshwa Tanzania.

MWISHO.

Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI