Header Ads Widget

IDADI YA VIFO KWENYE AJALI YA NDEGE YA INDIA YAFIKIA 270

 

Idadi ya vifo kwenye ajali mbaya ya ndege ya shirika la ndege la India imeongezeka hadi 270 siku ya Jumamosi, huku familia zikiwa na huzuni na hasira kutokana na kucheleweshwa kukabidhiwa miili ya wapendwa wao ambayo iliteketea vibaya katika ajali hiyo iliyotokea katika jiji la Ahmedabad, magharibi mwa India.

Ndege ya Boeing 787-8 Dreamliner iliyokuwa na watu 242 ndani yake ikielekea Uwanja wa Ndege wa Gatwick nchini Uingereza, ilianza kushuka ghafla sekunde chache baada ya kuruka siku ya Alhamisi na kusababisha mlipuko mkuwa wa moto pale ilipogonga majengo yaliyo chini, katika kile kinachotajwa kuwa janga baya zaidi la ndege duniani katika kipindi cha muongo mmoja.

Takribani miili 270 imetolewa kutoka eneo la ajali ya ndege, alisema Dhaval Gameti, rais wa Chama cha Madaktari Wanafunzi katika Chuo cha udaktari cha B.J., alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari.

Ni mtu mmoja tu kati ya abiria na wahudumu 242 waliokuwemo kwenye ndege hiyo ndiye aliyenusurika, huku wengine wote wakifariki dunia baada ya ndege hiyo kugonga bweni la chuo kikuu cha udaktari wakati ilipokuwa ikianguka.

Ndugu wenye wasiwasi wamekuwa wakingoja nje ya hospitali moja mjini Ahmedabad kukusanya miili ya wapendwa wao waliofariki kwenye ajali hiyo, huku madaktari wakifanya kazi kwa muda wa ziada kuchukua sampuli za meno kutoka kwa marehemu kwa ajili ya utambuzi na uchunguzi wa vinasaba (DNA)

Miili mingi katika ajali hiyo iliteketea vibaya kwa moto, na mamlaka zinatumia sampuli za meno kufanya uchunguzi wa utambuzi.

Jaishankar Pillai, daktari wa uchunguzi wa vinasaba wa meno, aliwaambia waandishi wa habari siku ya Ijumaa kuwa tayari walikuwa na rekodi za meno za wahanga 135 walioteketea kwa moto, ambazo zinaweza kulinganishwa na kumbukumbu za awali za meno za waathirika, picha za mionzi au rekodi nyingine.

Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI