Na Matukio Daima App.
DODOMA.Serikali imeendelea kutambua mchango wa walimu katika maendeleo ya sekta ya elimu kwani ni wazalishaji wa watalaamu mbalimbali waliopo katika sekta zote ikiwemo afya, nishati, sayansi na teknolojia. Sambamba na kufanya maboresho yatakayowaongezea walimu ari ya kufanya kazi kwa bidii, weledi, uadilifu na kutanguliza mbele maslahi ya Taifa.
Mafanikio yaliyopatikana katika sekta hiyo yanachangiwa moja kwa moja na walimu. Hivyo, Chama cha Walimu Tanzania (CWT) kina mchango mkubwa kwa jamii na kwa Taifa kwa ujumla kwa kuwa pamoja na jukumu la kufundisha na kujengea watu maarifa, mwalimu ni mzazi wa kiroho, kiongozi wa fikra, na ni mjenzi wa maadili katika jamii.
Hayo yameelezwa na Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati,Dkt. Doto Biteko Juni 8, 2025 jijini Dodoma wakati akimwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan katika ufunguzi wa Mkutano Mkuu wa Saba wa Chama Cha Walimu Tanzania (CWT).
Amesema katika kuimarisha sekta ya elimu ili kuongeza ufanisi na kusogeza huduma kwa jamii. Serikali imefanikiwa kujenga jumla ya madarasa 62,685 kwa shule za msingi na sekondari, shule za sekondari 1,031, shule mpya za msingi 1,580 na nyumba za walimu 1,792.
Ameongeza kuwa katika kipindi cha mwaka 2020/21 hadi 2024/25, Serikali imefanikiwa kuwalipa malimbikizo ya mishahara walimu 101,596, kulipa watumishi 156,556 madeni yasiyo ya mishahara na kuongeza mshahara kwa watumishi wa umma ambapo kima cha chini kuanzia mwezi Julai, 2025 kitakuwa shilini 500,000 badala ya 370,000.
"Serikali inaendelea kutoa ajira za walimu ambapo kuanzia mwaka 2021 hadi sasa, jumla ya walimu 40,527 wameajiriwa katika maeneo mbalimbali nchini. Lengo la kufanya hivi ni kutatua changamoto mbalimbali zilizopo," amesema Dkt. Biteko.
Dkt Biteko amepongeza matokeo ya zoezi la 'Samia Teachers Mobile Clinic' kwa kuwafikia walimu 48,380 pamoja na kutatua kero zao huku akiwaomba kuongeza ubunifu utakaowawezesha kuwa na mikakati mingine yenye lengo la kuimarisha utendaji katika sekta ya elimu na kushirikiana na Serikali kwa kutekeleza miradi ya Elimu ya TEHAMA kwa walimu na miradi mingine isambae kwenye mikoa yote nchini.
MWISHO.
0 Comments