Header Ads Widget

Dk. Nchimbi awasisitiza Wafugaji kuzingatia Sheria.


Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Balozi Dk. Emmanuel Nchimbi, akiongea kwenye Kongamano la Wafugaji lililofanyika viwanja vya Nanenane Nyakabindi Mkoani Simiyu.


Na COSTANTINE MATHIAS, Simiyu.


WAFUGAJI nchini wametakiwa kuzingatia sheria ili kudhibiti Migogoro iliyokuwepo ya kuingiza Mifugo Hifadhini pamoja na ya Wakulima ambayo ilisababisha kuwepo kwa kesi nyingi mahakamani 


Hayo yamebainishwa leo na Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Balozi Dk. Emmanuel Nchimbi wakati akihitimisha Kongamano la Wafugaji lililofanyika katika viwanja vya Nanenane Nyakabindi Mkoani Simiyu huku akiwasisitiza Wafugaji kufuata Sheria katika maeneo yaliyozuiwa kwa Mujibu wa Sheria.


Aidha, Balozi Dk. Nchimbi ameelekeza Ofisi ya Waziri Mkuu, kuhakikisha wanaratibu na kurejesha Mifugo ya Wafugaji waliokuwa wameshinda kesi mahakamani kwa mujibu wa Sheria.


"Wafugaji zingatieni Sheria ili kuepusha migogoro, Nilitoa maelekezo kwa serikali ya kulipa fidia, nitumie kongamano hili kuielekeza Ofisi wya Waziri Mkuu kuratibu jambo hili na kufika mwisho" amesema Balozi Dk. Nchimbi.



Awali Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Dk. Ashatu Kijaji amesema Wizara hiyo inatekeleza majukumu yake na imeweka kipaumbele cha kushirikiana na wadau wanaozalisha mazao ya Mifugo.



Waziri huyo amewataka Wafugaji kutambua Umuhimu wa Chanjo ya Kitaifa ya mara moja na pamoja na Utambuzi wa Mifugo, kampeni ambayo inatarajia kuzinduliwa na Rais Dk. Samia Suluhu Hassan ambaye Mgeni Rasmi na kwamba zoezi hilo litatekelezwa kwenye Halmashauri 184 nchini.


"Wafugaji bado tuna kazi ya kufanya kuyafikia Malengo yaliyoelekezwa kwenye ilani ya CCM, Rais ametufanyia makubwa Wafugaji ikiwemo kutafuta masoko ili tufuge kibiashara kwa lengo la kulisha Viwanda vyetu" amesema Waziri huyo.



Awali Katibu wa Chama cha Wafugaji Tanzania (CCWT), Mathayo Daniel ameiomba serikali kuwatengea maeneo ya malisho ya mifugo na kisha kuyamilikisha kwa wafugaji ili kuondoa migogoro kati yao na wakulima.



Katibu huyo ameeleza kuwa miongoni mwa kero zinazowafanya wafugaji kuhamahama ni pamoja na kutafuta malisho ya uhakika na maji kwa ajili ya mifugo yao.



Amesema kuwa licha serikali kuhakikisha sekta ya mifugo inasimama kwa kujenga majosho 750 ya kuogeshea mifugo na baadhi ya maeneo kuchimbiwa visima vya maji ambavyo havitoshi lakini bado wafugaji wanahangaika kutafuta malisho ya mifugo yao.



Amesema kuwa kumekuwa na migogoro ya mara kwa mara hapa nchini kati ya wakulima na wafugaji kwa ajili ya kugombea maeneo kwa ajili ya malisho na kusababisha madhara makubwa na hata vifo.



"Pamoja na mambo mazuri ambayo serikali yetu imetufanyia,ombi letu la sasa ni maeneo ya malisho yapimwe na yamilikishwe kwa wafugaji lakini pia tupatiwe maji ya mifugo," amesema na kuongeza.



"Unajua kero kubwa inayosababisha wafugaji kuhamahama kutoka eneo moja kwenda jingine ni malisho na maji,wafugaji wakipata vitu hivyo ile migogoro ya maeneo kati yao ya wakulima itamalizika na amani itakuwepo kwa makundi hayo,"amesema.


Mwisho.














Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI