Header Ads Widget

BODI YA TFS YAIPONGEZA WEST KILIMANJARO KWA MCHANGO WANE WA KIUCHUMI. A KIJAMII



Na Mwandishi Wetu – Siha, Kilimanjaro


Bodi ya Ushauri ya Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) imepongeza utendaji bora wa Shamba la Miti la West Kilimanjaro, huku ikielezea kuridhishwa na namna linavyoboresha maisha ya wananchi na kuchangia maendeleo ya Taifa kupitia uzalishaji endelevu wa mazao ya misitu.

Akizungumza kwa niaba ya Mwenyekiti wa Bodi hiyo, Meja Jenerali Dkt. Mbaraka Mkeremy, wakati wa ziara ya kikazi iliyofanyika Juni 24, 2025, Mjumbe wa Bodi Dkt. Siima Bakengesa alisema kuwa Shamba hilo limeonyesha mfano wa kuigwa katika kuendeleza rasilimali za Taifa kwa manufaa ya wananchi na kizazi kijacho.

"Tumefurahishwa na kazi nzuri inayofanyika hapa West Kilimanjaro. Tumeona namna shamba hili linavyochangia pato la Taifa kupitia uzalishaji wa miti na pia kuwanufaisha wananchi kwa kuwashirikisha katika shughuli mbalimbali za kiuchumi kama kilimo na ufugaji wa nyuki,” alisema Dkt. Bakengesa.

Dkt. Bakengesa alisifu uwekezaji unaoendelea kufanyika katika kuboresha mazingira ya kazi kwa watumishi, ikiwemo ujenzi wa nyumba za makazi, ukarabati wa majengo na uboreshaji wa miundombinu ya msingi.




"Tunapongeza juhudi za TFS katika kuboresha mazingira ya kazi kwa watumishi. Haya ni mambo muhimu yanayochochea ufanisi na kuongeza motisha kazini,” aliongeza.

Kwa upande wake, Mhifadhi Mkuu wa Shamba hilo, Bw. Robert Faida, alieleza kuwa shamba hilo limeendelea kutekeleza miradi ya kimkakati ya uwekezaji kwa kushirikiana kwa karibu na makao makuu ya TFS.

"Katika miaka ya hivi karibuni, tumeimarisha huduma mbalimbali ikiwa ni pamoja na miundombinu ya makazi, vitendea kazi, na ushirikiano na jamii. Tunaendelea kuboresha zaidi kwa kadri rasilimali zinavyoruhusu,” alisema.




Akizungumzia nafasi ya sekta binafsi katika kuendeleza misitu, Bw. Faida alihimiza wawekezaji kuanzisha viwanda vya kisasa vya kuchakata mazao ya misitu, huku akieleza kuwa mahitaji ya mbao nchini yanaendelea kuongezeka na kutoa fursa pana kwa uwekezaji.

"Tunakaribisha sekta binafsi kuwekeza katika teknolojia kama finger jointing na fiberboard ili kuongeza thamani ya mazao ya misitu, kupunguza upotevu wa malighafi na kuongeza ajira,” alisema.

Bodi hiyo pia ilieleza kufurahishwa na namna jamii zinazozunguka Shamba la West Kilimanjaro zinavyoshirikishwa katika shughuli za kiuchumi, ikiwa ni pamoja na kilimo cha viazi na karoti, pamoja na ufugaji wa nyuki katika maeneo maalum.

"Tunatambua mchango wa shamba hili katika kuboresha maisha ya wananchi wa maeneo ya jirani. Ushirikiano huu unajenga msingi imara wa utunzaji wa rasilimali za misitu kwa pamoja,” alisema Dkt. Bakengesa.

Dkt. Bakengesa alisisitiza umuhimu wa kuweka wazi takwimu za uzalishaji na ushiriki wa jamii, ili kuongeza uwazi na kufanikisha utekelezaji wa Mpango wa Kitaifa wa Urejeshwaji wa Ardhi Iliyoharibika (5.2 milioni ha).

"TFS ni miongoni mwa taasisi muhimu katika kutekeleza mpango huu wa kitaifa. Tunashauri kila miche inayogawiwa kwa jamii na taasisi ifuatiliwe ili kupima matokeo kwa usahihi,” alibainisha.


Bodi ya Ushauri ya TFS imesisitiza dhamira yake ya kuendelea kutoa ushauri wa kitaalamu ili kuboresha zaidi mazingira ya kazi, kuongeza uzalishaji, na kuimarisha ushirikiano wa TFS na jamii zinazozunguka mashamba.


"Tutaendelea kushirikiana kwa karibu na Menejimenti ya TFS ili kuhakikisha rasilimali za Taifa zinatunzwa kwa tija, kwa faida ya kizazi cha sasa na kijacho,” alisema Dkt. Bakengesa.

Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI