WAZIRI wa Madini Mhe. Anthony Mavunde aliweka wazi mafanikio 16 ya Sekta ya Madini katika kipindi cha Miaka Minne ya Rais Samia Suluhu Hassan ikiwemo Benki Kuu ya Tanzania kununua Tani 3.7 kwa gharama ya Shilingi 702.3 Bilioni.
Akizungumza na Waandishi wa Habari Mei 15, 2025, katika ukumbi wa Idara ya habari (MAELEZO), Waziri Mavunde alisema kati ya kiasi kilichonunuliwa takribani, Kilo 2,954 zilisafishwa katika viwanda vya kusafisha dhahabu vilivyoko nchini.
Mhe. Mavunde alisema katika Bara la Afrika nchi tano zinazofanya vizuri katika ununuzi wa dhahabu, Tanzania ipo huku nchi ya Algeria ikiongoza.
“Miaka mingi nchi yetu iliacha kununua dhahabu kupitia Benki Kuu, lakini mwaka wa fedha 2024/2025 tulifanya marekebisho ya Sheria ya Madini kifungu cha 59 sura ya 123 ambacho kinampa dhamana Waziri wa Madini kujadiliana na wamiliki wa leseni kutenga asilimia 20 ya madini yanayozalishwa na kuchakatwa ndani ya nchi kuyeyushwa na kusafishwa kununuliwa na BOT ili kukuza hifadhi ya fedha za kigeni kupitia ‘monetary gold’ ambayo ina manufaa makubwa kwa ukuaji na ustahimilivu wa Uchumi wa Taifa,” amesema Waziri Mavunde na kusisitiza:
“Nchi inayoongoza Afrika kwa kuwa na hifadhi kubwa ya dhahabu ni Algeria, katika kumi bora kwenye orodha ilikuwa ni Msumbiji wana tani 3.6, sisi Tanzania tumeanza kununua dhahabu Oktoba 1, 2024 mpaka sasa Tani 3.7 tumeshampiku aliyekuwa kumi bora na huu ndio mwanzo ni miezi nane tu, miaka mitano ijayo tutakuwa mbali,” amesema.
Serikali kupitia Benki Kuu ya Tanzania (BoT) ilianza rasmi ununuzi wa dhahabu Oktoba 1, 2024, kupitia viwanda vitatu vya kusafisha dhahabu vya MPMR (Mwanza), GGR (Geita), na Eyes of Africa (Dodoma).
Aidha, alisema mkakati wa Wizara ya Madini ni kuhakikisha Serikali kupitia Benki Kuu, inaangalia uwezekano wa kuanzisha uuzaji wa sarafu za dhahabu zenye uzito ili kuwaongezea watanzania wigo wa uwekaji akiba na uwekezaji kupitia ununuzi wa dhahabu.
“Vilevile hatua hii itaongeza umiliki wa dhahabu miongoni mwa wananchi, kuimarisha soko la ndani la dhahabu, na kuimarisha mzunguko wa fedha ndani ya nchi,” alisema Mhe. Mavunde.
*Uongezaji Thamani Madini*
Waziri Mavunde alisema tayari kuna jumla ya viwanda 8 vya kusafisha dhahabu nchini na hivi sasa Serikali inavisaidia kuweza kukidhi viwango vya kimataifa na kuongeza kwamba, tayari Serikali imetenga eneo maalum la uwekezaji kwa ajili ya viwanda vya uongezaji thamani madini na bidhaa zinazotumika migodini la Buzwagi Special Economic Zone mahali ulipokuwa mgodi mkubwa wa uchimbaji dhahabu Buzwagi na kueleza kwamba, hadi sasa tayari viwanda kadhaa vimeanza kazi ikiwemo cha kutengeneza vipuri cha East African Conveyor Supplies Limited (EACS), huku kiwanda cha kusafisha madini ya metali cha kampuni ya Tembo Nickel Refining Company Limited.
*Ununuzi wa Mafuta na Fedha za Kigeni kutumia Dhahabu*
Waziri Mavunde alisema pia, Serikali kupitia Benki Kuu, itafikiria kuanzisha utaratibu wa kutumia dhahabu itakayonunuliwa, hususan isiyokidhi vigezo vya kuingia katika soko la LBMA, kubadilishana na nishati ya mafuta (barter trade) na kununulia fedha za kigeni kulingana na mahitaji ya nchi.
*Ununuzi wa Fedha za Kigeni zinazotokana na Mauzo ya Madini*
Waziri Mavunde alisema sheria inayotaka kampuni na wafanyabiashara kurejesha fedha zinazotokana na mauzo ya bidhaa nje ya nchi, ikiwemo madini, itaendelea kusimamiwa ipasavyo.
“Iwapo Serikali itaipa Benki Kuu ya Tanzania haki ya kwanza (Pre-emption right) ya kununua fedha hizo zinazorejeshwa nchini na kuwalipa wahusika kwa Shilingi ya Tanzania itasaidia upatikanaji wa fedha za kigeni na kuimarisha umadhubuti wa shilingi na viwango vya ubadilishaji fedha,” alisema Waziri Mavunde.
*#InvestInTanzaniaMiningSector*
*#Mining4Development*
*#Vision2030: MadininiMaishanaUtajiri*
0 Comments