Na Hamida Ramadhan, Matukio Daima – Dodoma
WAZIRI wa Uchukuzi, Prof. Makame Mbarawa, amesema kuwa serikali imetunga sheria mahsusi ili kuwezesha ushiriki wa sekta binafsi katika ujenzi na uendeshaji wa miradi mikubwa ya kiuchumi, hususan katika sekta ya miundombinu.
Akizungumza na waandishi wa habari Bungeni jijini Dodoma, Prof. Mbarawa alisema kuwa sekta binafsi ni injini muhimu katika maendeleo ya nchi, na bila ushiriki wake, sekta ya miundombinu haiwezi kuendelea kwa kasi inayotakiwa.
“Kwa kuliona hilo, tumeweka sheria inayoruhusu sekta binafsi kushiriki kwenye utekelezaji wa mradi wa reli ya kisasa (SGR), hasa katika usafirishaji wa mizigo,” alisema.
Aliongeza kuwa kuanzia mwishoni mwa Juni mwaka huu, usafirishaji wa mizigo kupitia reli kutoka Dar es Salaam hadi Dodoma utaanza rasmi, na kuitaka sekta binafsi kuchangamkia fursa hiyo kwa kuwekeza katika usafirishaji wa mizigo.
“Bila sekta binafsi hatuwezi kufika mbali. Tunaona mafanikio katika Bandari ya Katavi ambako kampuni ya Kichina inatekeleza ujenzi – hii ni ishara kuwa sekta binafsi ndio injini ya maendeleo,” alieleza Prof. Mbarawa.
Aidha, alimshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa mafanikio makubwa yanayoonekana katika mradi wa SGR na kuahidi kuwa vipande vilivyobaki vya mradi huo vitakamilika kwa kasi kubwa.
Kuhusu sekta ya anga, Waziri Mbarawa alisema kuwa bajeti ya mwaka wa fedha 2025/2026 imetenga Shilingi bilioni 246 kwa ajili ya ununuzi wa ndege mpya, na Shilingi bilioni 87 kwa ajili ya ukarabati wa viwanja vya ndege ili kuimarisha sekta ya utalii.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Reli Tanzania (TRC), Mhandisi Masanja Kadogosa, alisema kuwa ujenzi wa reli ya kisasa unaendelea vizuri, na TRC iko tayari kutoa huduma bora na za kisasa kwa Watanzania wote. Alibainisha kuwa uboreshaji wa miundombinu hiyo umechochea ongezeko kubwa la wateja, jambo linaloonyesha imani ya wananchi kwa huduma za reli.
“Kwa sababu ya wingi wa wateja, tunafikiria kuongeza safari za treni kati ya Dodoma na Dar es Salaam, hasa kuanzia Ijumaa hadi Jumatatu ambapo mahitaji ni makubwa sana,” alisema.
Aliongeza kuwa TRC inaendelea kujiimarisha kwa kuongeza idadi ya mabehewa na treni mpya ili kuhakikisha kuwa kila Mtanzania anapata huduma kwa wakati na kwa viwango vya juu vya usalama na ufanisi
0 Comments