Header Ads Widget

WAZIRI CHANA AZINDUA MRADI WA DOLA MILIONI 5.8 KUHIFADHI MISITU YA ASILIA

 


Na Matukio Daima App.

Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Balozi Dkt. Pindi Chana (Mb), amezindua  mradi wa 'Kuimarisha Ustahimilivu wa Bioanuai ya Misitu ya Mazingira Asilia Tanzania dhidi ya Athari za Mabadiliko ya Tabianchi', wenye thamani ya Dola za Kimarekani 5.8 milioni.

 Mradi huo umefadhiliwa na Mfuko wa Mazingira Duniani (GEF) kwa kushirikiana na Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP).

Uzinduzi huo umefanyika leo, Mei 5, 2025, katika Msitu wa Hifadhi ya Mazingira Asilia wa Pugu–Kazimzumbwi, wilayani Kisarawe, mkoa wa Pwani, sambamba na uzinduzi wa Mkakati wa Kuokoa Ardhi ya Misitu Iliyoharibika.



Akizungumza katika hafla hiyo, Mhe. Chana amesema mradi huo unalenga kuongeza ustahimilivu wa misitu dhidi ya athari za mabadiliko ya tabianchi kwa kuimarisha mifumo ya ulinzi, kusaidia shughuli rafiki kwa mazingira kama vile utalii, na kuimarisha mipaka, vituo vya ulinzi, pamoja na vifaa vya kukabiliana na majanga kama moto wa msituni.

Aidha, amesema mradi utasaidia jamii zinazozunguka misitu kwa kuwapatia shughuli mbadala za kiuchumi zitakazosaidia kupunguza utegemezi wa moja kwa moja kwenye misitu.

“Mradi huu wa miaka sita, kuanzia Septemba 2023 hadi 2029, unatekelezwa kwa ufadhili wa GEF na UNDP kwa gharama ya Dola za Kimarekani 5,837,010,” amesema Mhe. Chana.

Amesema mradi huo utatekelezwa katika misitu tisa ya hifadhi iliyoko kwenye mikoa mitano: Hassama Hills, Nou na Mlima Hanang (Manyara), Uzigua na Pugu–Kazimzumbwi (Pwani), Pindiro na Rondo (Lindi), Mwambesi (Ruvuma) na Essimingor (Arusha).


Waziri Chana ameeleza kuwa utekelezaji wa mradi utasaidia kuimarisha uwezo wa hifadhi hizo kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi, kuongeza mapato ya Serikali kupitia TFS, kuimarisha ushirikiano kati ya Serikali na jamii za jirani na kujenga uthabiti wa mifumo ya ikolojia kwa kuunganisha hifadhi za mazingira asilia na maeneo mengine ya uhifadhi.

Aidha, Waziri amewapongeza wadau wa maendeleo na asasi za kiraia kwa mchango wao mkubwa katika juhudi za Serikali za kuhifadhi misitu, na kusisitiza umuhimu wa kuendeleza ushirikiano huo kwa manufaa ya taifa na vizazi vijavyo.

Kwa upande wake, Katibu Mkuu Wizara ya Maliasili na Utalii, Dkt. Hassan Abbasi amesisitiza juu ya wananchi kutunza na kuhifadhi maliasili za misitu huku akitoa onyo kwa wanaokiuka taratibu za uhifadhi kuchukuliwa hatua kali.

Naye Mwakilishi Mkazi wa Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP), Shigeki Komatsubara  amesema mradi huo ni muhimu kwa Tanzania kutokana na athari mbambali zinazoikumba misitu ikiwemo mabadiliko ya tabianchi, uchomaji moto hivyo utasaidia kuirisha maisha ya na vipato vya wananchi kwa kuacha kutegemea misitu.


Hafla hiyo imehudhuriwa na viongozi kutoka Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Wizara ya Fedha, TAMISEMI, wilaya ya Kisarawe, Wizara ya Maliasili na Utalii, TFS, pamoja na wadau wa maendeleo.

MWISHO.

Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI