Header Ads Widget

TAMKO LA KUFUNGULIWA MPAKA WA MALAWI LAREJESHA MATUMAINI KWA WAFANYABIASHARA WA MAZAO ILEJE.

 

Na Moses Ng'wat, Ileje

WAFANYABIASHARA wa mazao katika mpaka wa Isongole, Wilaya ya Ileje mkoani Songwe, wameeleza furaha yao kufuatia kufunguliwa kwa mpaka kati ya Tanzania na Malawi, uliokuwa umefungwa kwa muda kutokana na mvutano uliosababishwa na vikwazo vya kibiashara.

Wakizungumza katika mpaka wa Isongole, Wilayani Ileje, wafanyabiashara hao wamesema hatua hiyo imeleta ahueni kubwa kwa wananchi na wafanyabiashara wa pande zote mbili, waliokuwa wameathirika kwa kiasi kikubwa kutokana na kufungwa kwa mpaka huo.

Mwenyekiti wa wafanyabiashara wa mazao katika mpaka huo, Bosco Siame, ambaye pia ni mfanyabiashara wa nafaka katika soko la Isongole, amesema kipindi chote cha kufungwa kwa mpaka kiliwasababishia hasara kubwa kwani walishindwa kusafirisha bidhaa wala kufanya biashara ya kuvuka mpaka.

Newadi Cheyo, mfanyabiashara wa pembejeo, amesema hali ya maisha kwa wakazi wa maeneo ya mpakani ilibadilika kwa kiwango kikubwa, huku mwingiliano wa kijamii na kiuchumi ukipotea.

"Hali ilikuwa mbaya kwani ilifika wakati mtu hata akinunua hata kilo moja ya mchele kutoka Tanzania alikuwa haruhusiwi kuingia nayo Malawi... maofisa mpakani walikuwa wakali na kumwambia kama anataka kula wali ni bora arudi kupikia Tanzania na kula huku huku, kisha avuke mpaka akiwa ameshiba!" alisimulia Cheyo kwa masikitiko.

Aliongeza kuwa hata bidhaa kutoka Malawi kama vile mayai na kuku hazikuruhusiwa kuingia upande wa Tanzania, hali iliyozua sintofahamu na kuyumba kwa biashara ndogondogo ambazo hutegemea mwingiliano wa bidhaa baina ya nchi hizo.



Kwa upande wake, Daurd Kayinga, mfanyabiashara mwingine, amesema hali ya biashara imeanza kuimarika hatua kwa hatua tangu kufunguliwa kwa mpaka huo, na kuishauri serikali kuhakikisha migogoro ya kibiashara ya namna hiyo haitokei tena bila taarifa wala maandalizi kwa wananchi.

Awali, Tanzania kupitia Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe, ilitangaza kuchukua hatua kali dhidi ya Malawi na Afrika Kusini kutokana na kile kilichoelezwa kuwa ni vikwazo vya kibiashara vilivyowekwa dhidi ya bidhaa za Tanzania.

Hatua hizo zilijumuisha: kuzuia uingizwaji wa bidhaa zote za kilimo kutoka Malawi na Afrika Kusini hadi masoko yao yatakapofunguliwa kwa bidhaa za Tanzania; kuzuia bidhaa hizo kupitishwa ndani ya Tanzania au kutumia Bandari ya Dar es Salaam; na pia kusitisha usafirishaji wa mbolea kwenda Malawi kama njia ya kulinda maslahi ya wakulima wa ndani.

Hata hivyo, serikali za Tanzania na Malawi zilifikia mwafaka na kuafikiana kufungua tena mpaka huo baada ya mkutano wa mawaziri wa nchi hizo uliofanyika Mei 2, 2025 jijini Dodoma.

Wafanyabiashara wa Isongole na maeneo ya jirani sasa wameanza kurejea kwenye shughuli zao za kiuchumi huku wakiwa na matumaini makubwa kuwa ushirikiano wa kibiashara kati ya Tanzania na Malawi utaimarika zaidi, hivyo kuinua uchumi wa wananchi wa maeneo ya mipakani ambao hutegemea kwa kiasi kikubwa biashara za kuvuka mpaka.

Mwisho.

Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI