Wananchi mkoani Kagera wametakiwa kutumia fursa ya uwepo wa Madakatari Bingwa zinazoendelea mkoani humo na kuacha visingizio vya imani za kishirikina, badala yake kufika hospitali kupata huduma za Kibingwa zinazotolewa na Kambi ya Madaktari Bingwa na Bobezi wa Rais Samia zinazoendelea kwa siku tano katika hospitali ya mkoa.
Mkuu wa mkoa wa Kagera Bi. Fatma Mwassa ametoa wito huo leo Mei 5, 2025 wakati wa ufunguzi wa kambi rasmi ya madaktari wa huduma za Mkoba zilizoanza kwenye ngazi ya Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Kagera.
"Watu wanaumwa lakini hawana utamadumi wa kupima Afya zao mara kwa mara ili kujua ugonjwa walio nao badala yake wanasingizia kurogwa," amesema Mhe. Fatma Mwassa na kuongeza.
"Ndugu zangu watu tunaumwa, unajisikia sehemu ya mwili inauma taratibu unasema nimerogwa kumbe hujarogwa ni ugonjwa tu, njoo hospitali utibiwe usiache ugonjwa ukuletee madhara makubwa," amesisisitiza Mkuu wa mkoa wa Kagera.
Aidha Mkuu huyo wa Mkoa wa Kagera amewataka wakazi hao kutambua kwamba wanaumwa na wachukue fursa ya uwepo wa madaktari hao kuwapunguzia gharama za kwenda hospitali zilizo mbali kufuata huduma ambazo sasa zimeletwa karibu na wananchi.
Kwa upande wake Mratibu wa zoezi hilo kutoka Wizara ya Afya Dkt. John Mwimbeki akiongea na vyombo vya habari nje ya mkutano wa uzinduzi wa kambi hiyo amesema faida kubwa ya uwepo madaktari bingwa na bobezi mkoani kagera ni kuwezesha wagonjwa kupata huduma za matibabu mbalimbali zinazotolewa na madaktari hao.
"Unaweza kufika hospitali unaumwa sikio lakini ukagundulika kuwa na tatizo la mkojo au figo utapata matibabu yote kwa mara moja kutoka kwa kila mtaalam wa ugonjwa unaoumwa kwakuwa kuna madaktari bingwa wa nyanja mabalimbali za kitabibu," ameongeza Dkt. Mwombeki.
Nanye Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa, Bukoba Dkta. Museleta Nyakiroto amesema kuwa katika kambi hiyo wanategemea kuona wananchi 2500.
0 Comments