Na COSTANTINE MATHIAS, Igunga.
WAKULIMA wa Pamba kutoka vijiji vya Mbutu na Mwang'halanga, wilayani Igunga Mkoani Tabora, wameipongeza serikali kwa kuleta Maafisa Ugani kupitia Mpango wa Jenga Kesho Bora (BBT) ambao wameongeza Elimu ya Kilimo na matumizi ya Pembejeo kwa wakulima hao walipokuwa wanawatembelea mashambani.
Aidha, wamesema kupitia Elimu waliyopatiwa katika uzalishaji wa zao la Pamba, wakulima hao wanatarajia kuongeza tija, kupata mavuno mengi na Pamba safi tofauti na ilivyokuwa awali kabla ya ujio wa Maafisa Ugani hao miaka ya nyuma.
Wakizungumza na Waandishi wa Habari kwenye mashamba ya wakulima hao, wamesema Maafisa Ugani wa BBT wameanza kuwafikia wakulima mashambani moja kwa moja tofauti na miaka ya nyuma walipokuwa wanalima kwa kubuni pasipo kuwa na utaalamu wowote.
Lucia Luhende, mkulima wa Pamba kijiji cha Mwang'halanga anaishukuru serikali kuongeza Maafisa Ugani kupitia BBT ambao wanashuka vijijini kutoa Elimu ya Kilimo Bora cha Pamba na kwamba katika msimu huu wanatarajia kupata mavuno ya kutosha.
"Tunashukuru serikali kwa jitihada za kupambania Kilimo cha Pamba, tumepata Madawa kwa wakati pia tumeelimishwa juu ya kulima kwa mistari kwani miaka ya nyuma tulikuwa tuna panda zigizaga...BBT wametusimamia kwa hatua zote toka kuandaa shamba, kulima, kupanda, kupalilia, kupunguza Miche, kupulizia wadudu na kuvuna" amesema.
Mkulima mwezeshaji kutoka Kijiji cha Mwang'halanga, Jackson Charles anasema ujio wa BBT umewafanya wakulima kulima kisasa kwani wamekuwa wakifuatiliwa kila hatua ya kulima Pamba na pia wamepata Pembejeo kwa wakati.
Christina Salum, mkulima wa Pamba kutoka Kijiji cha Mbutu amesema wanatarajia kupata mavuno ya kutosha kupitia Elimu waliyopata kwa Maafisa Ugani wa serikali kupitia Mpango wa BBT.
Tigana Lazaro, mkulima wa Kijiji cha Mbutu amesema Maafisa Ugani wa BBT wamewasaidia wakulima na kuwawezesha kupanda kwa wakati pia kuwapatia Elimu sahihi ya matumizi ya Pembejeo.
Ameipongeza serikali kupitia Bodi ya Pamba Tanzania (TCB) kwa kuendelea kusimamia zao hilo kuja na Mpango huo ambao umesuluhisha changamoto za upotevu wa dawa pia Maafisa Ugani hao wamepata takwimu sahihi za wakulima sababu wanawatembelea mashambani mara Kwa mara.
Mwisho.
0 Comments