Header Ads Widget

WAKULIMA MASWA WATAKIWA KULIMA ZAO LA ALIZETI KWA UBORA.


Mtaalam wa mazao ya biashara,Mbayani Mollel akionyesha alizeti iliyokomaa katika shamba la mfano katika kijiji cha Buyubi wilaya ya Maswa.


Na Samwel Mwanga,  Maswa.


WAKULIMA wa zao la alizeti wametakiwa kuzingatia viwango vya ubora wa uzalishaji ili kuongeza thamani ya mazao yao na kuvutia masoko ya ndani na nje ya nchi.


Afisa kilimo wa wilaya ya Maswa,Masalu Lusana amesema hayo Mei 7,2025 wakati wa mafunzo ya kilimo bora kwa wakulima wa alizeti yaliyofanyika katika kijiji cha Buyubi wilayani humo.


Amesema wakulima wengi wamekuwa wakikosa soko la uhakika kutokana na kutokufuata kanuni bora za kilimo na uhifadhi wa mazao baada ya kuvuna.


Amesema kuwa serikali imefungua fursa kwa wadau mbalimbali  kusaidia katika sekta ya kilimo ikiwemo ya uzalishaji wa mbegu bora za alizeti kwa lengo la kuhakikisha mkulima anapata mazao ya kutosha na yenye ubora.

“Tunawasihi wakulima wazingatie matumizi ya mbegu bora,matumizi sahihi ya pembejeo na kuhifadhi alizeti kwa njia salama ili kupunguza uchafuzi unaoathiri ubora wa mafuta yanayozalishwa,” amesema.


Amesema kuwa serikali kupitia mpango wa Maendeleo ya Sekta ya Kilimo awamu ya pili (ASDP II)inalenga kuongeza uzalishaji wa mazao ya mafuta kwa kuwajengea uwezo wakulima, kuimarisha utafiti na kusambaza teknolojia bora ya kilimo.


“Mpango huo unasisitiza ushirikiano kati ya sekta ya umma na binafsi katika kufanikisha mapinduzi ya kilimo cha mazao ya mafuta, ikiwemo alizeti,”amesema.


Atilio Mbwilo ni Mratibu wa mradi wa Vijana, kilimo biashara katika wilaya ya Maswa na Meatu,ambao uko chini ya Shirika lisilo la kiserikali la Brac Maendeleo Tanzania amesema kuwa kupitia mradi huo moja ya malengo ni pamoja na kukuza mnyororo wa thamani ya zao hilo pamoja na kutoa mbegu bora kwa wakulima zinazostahimili ukame.


“Kupitia mradi huu tunalenga kuwabadilisha wakulima kutoka kilimo cha kujikimu kwenda kilimo biashara kwa kuongeza tija na kupunguza upotevu wa mazao baada ya mavuno,”amesema.


Amesema kuwa katika kuhakikisha vijana na wanawake wananufaika na mradi huo wameanzisha mafunzo biashara ili kuhakikisha mbegu za zao hilo zinazopandwa zinakuwa na bora na kukomaa kwa muda mfupi hivyo wameanzisha mashamba darasa katika vijiji vinavyoteleza mradi huo.


“Ili tuweze kuwapatia wakulima wetu mbegu zilizo bora na hasa tuliowalenga ambao ni wanawake na vijana tumeanzisha shamba darasa la mbegu katika vijiji tunavyoteleza mradi wetu ila katika  kijiji cha Buyubi hapa tuna shamba bora la mfano na mbegu hizi tulizipata kwa kushirikiana na wenzetu wa SeedCo kwa kuzalisha mbegu hii aina ya LG 50745 ambayo katika maeneo yetu inastawi vizuri na kutoa mazao mengi kwa kipindi kifupi na inavumilia ukame,”amesema.


Mtaalamu wa mazao ya biashara,Mbayani Molel amesema ili wakulima wa alizeti waweze kunufaika na zao hilo ni lazima waendane na mabadiliko ya kisayansi na teknolojia katika uzalishaji na usindikaji.


“Uzalishaji wa alizeti unahitaji kuzingatia mnyororo mzima wa thamani kuanzia shambani hadi sokoni, ni muhimu wakulima wapatiwe elimu ya mara kwa mara kuhusu viwango vya ubora vinavyohitajika sokoni,” amesema.


Kwa upande wake, Meneja wa Kampuni ya ABC ya mjini Maswa, Yusuph Hamza inayojishughulisha na usindikaji wa mafuta ya alizeti, amesema baadhi ya wakulima wamekuwa wakileta alizeti yenye viwango vya chini kutokana na kutokukausha vizuri  hali inayosababisha hasara kwa mkulima.


“Kiwanda kinapokea tani nyingi za alizeti, lakini asilimia kubwa huwa na ubora wa chini,tunawahamasisha wakulima wazingatie usafi na uhifadhi sahihi ili kuongeza thamani ya mazao yao na kukidhi mahitaji ya soko,” amesema.


Juma Sende ni mkulima wa kijiji cha Buyubi anasema kuwa ni vizuri elimu ya kilimo bora ikatolewa kwa wakulima wa zao hilo sambamba na kuwahamasisha kuhakikisha wanapanda mbegu bora ili waweze kupata bei nzuri ya mafuta yanayotokana na zao hilo.

 

“Tunatakiwa sisi wakulima kuona umuhimu wa kuunganisha nguvu zetu tukaunda vikundi katika kilimo hiki cha zao la alizeti na kuuza alizeti kwa pamoja,hii itatusaidia kupata bei nzuri na kuwapa motisha ya kufuata viwango vya ubora vinavyohitajika kwa wanunuzi wetu,” amesema.


Takwimu kutoka idara ya kilimo zinaonesha kuwa uzalishaji wa alizeti katika mkoa wa Simiyu umeongezeka kwa asilimia 15 mwaka huu, lakini kiwango cha ubora bado ni changamoto inayohitaji kushughulikiwa ili kufikia viwango vya soko la kimataifa.


MWISHO.


Sehemu ya wakulima wa kijiji cha Buyubi wilaya ya Maswa wakiangalia zao la alizeti katika shamba la mfano la mbegu bora.
Sehemu ya shamba darasa la zao la alizeti katika kijiji cha Buyubi wilaya ya Maswa.









Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI