Header Ads Widget

LUKUVI ACHUKUA FOMU YA UTEUZI UBUNGE JIMBO LA ISMANI, AANZA RASMI SAFARI YA KULINDA NAFASI YAKE

 

Na Matukio Daima Media, Iringa

Aliyekuwa Mbunge wa Jimbo la Ismani mkoani Iringa, William Vangimembe Lukuvi, leo  Jumapili amechukua fomu ya kuomba ridhaa ya wananchi kuendelea kulitumikia jimbo hilo, baada ya kuteuliwa na Halmashauri Kuu ya Taifa ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) kuwa mgombea wake katika uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika mwezi Oktoba mwaka huu.

Lukuvi, ambaye ni miongoni mwa wanasiasa wenye uzoefu na mchango mkubwa katika historia ya siasa za Tanzania, aliwasili katika ofisi ya Msimamizi wa Uchaguzi wa majimbo ya Ismani na Kalenga, Bi. Caroline Otieno, majira ya saa 6:55 mchana akifuatana na viongozi na wanachama wa CCM wilaya ya Iringa vijijini. Msafara wake uliongozwa na Katibu wa CCM Wilaya ya Iringa Vijijini, Sure Mwasanguti, pamoja na Katibu wa Itikadi na Uenezi wa wilaya hiyo, Anord Mvamba, huku kukiwa na viongozi wengine wa chama, wanachama na wafuasi waliokuwa wamebeba mabango na kuimba nyimbo za hamasa.

Mara baada ya kukabidhiwa mkoba maalum wenye fomu za kugombea ubunge pamoja na miongozo ya Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi, Lukuvi alionekana mwenye furaha kubwa na kuonyesha shukrani za dhati kwa chama chake, akisema uteuzi huo ni ishara ya imani kubwa waliyonayo ndani ya CCM na wananchi wa Jimbo la Ismani kwa uongozi wake.

"Ninashukuru CCM kwa kuendelea kuniamini. Safari hii si yangu peke yangu bali ni ya wananchi wa Ismani ambao tumeshirikiana bega kwa bega kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo kwa miaka mingi Naahidi kuendelea kuwatumikia kwa uadilifu, bidii na mshikamano mkubwa kama ilivyo desturi yangu."

Kwa mujibu wa ratiba ya uteuzi, Lukuvi ndiye mteule wa kwanza wa CCM kuchukua fomu ya ubunge katika Wilaya ya Iringa Vijijini, ambayo ina majimbo mawili ya uchaguzi; Ismani na Kalenga. Jimbo la Kalenga, kwa upande wake, limepata mgombea Jackson Kiswaga, ambaye naye analichukua fomu leo.

Hali hiyo imemfanya Lukuvi kuwa mwanasiasa wa kwanza kuanzisha rasmi safari ya kinyang’anyiro cha uchaguzi mkuu kwa upande wa CCM wilayani humo, hatua inayotafsiriwa na wachambuzi wa siasa kama "ishara ya kujiamini na maandalizi makini ya chama katika kuendeleza ushindi wake".

HISTORIA NA MCHANGO WA LUKUVI

William Vangimembe Lukuvi ni jina linalotambulika vizuri katika siasa za Tanzania ameshika nyadhifa mbalimbali serikalini na ndani ya CCM, ikiwemo kuwa Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, nafasi aliyoitumia kusimamia mageuzi na maboresho makubwa katika sekta ya ardhi nchini.

Katika Jimbo la Ismani, ambako amekuwa mbunge kwa vipindi kadhaa, Lukuvi ametekeleza miradi mingi mikubwa ya maendeleo ambayo imeacha alama kwa wananchi. Miradi hiyo inajumuisha:

Uboreshaji wa huduma za afya: Kujenga na kukarabati zahanati na vituo vya afya, kuhakikisha upatikanaji wa dawa na vifaa tiba, na kusimamia ujenzi wa majengo mapya ya wodi na nyumba za watumishi wa afya.

Elimu: Kupitia nguvu za wananchi na michango ya serikali, shule kadhaa zimeboreshwa kwa kujengewa madarasa, mabweni, maabara na vyoo bora.

Miundombinu ya barabara: Lukuvi amesimamia barabara muhimu za vijijini na barabara kuu za uchumi zinazounganisha Ismani na maeneo jirani, jambo lililochangia kupunguza changamoto za usafiri na kukuza biashara.

Miradi ya umwagiliaji: Katika eneo la Pawaga  lenye rutuba kubwa, Lukuvi amekuwa kinara wa kupigania mabonde ya kilimo kuwekewa miundombinu ya kisasa ya umwagiliaji, hatua iliyosaidia kuongeza tija kwa wakulima na mapato ya familia.

Kwa mchango huo, Lukuvi anaingia tena uwanjani akiwa na akiba kubwa ya kazi za kimaendeleo zinazowabeba wananchi na kumpa nguvu mpya katika kampeni zake.

MCHANGO WA CCM KITAIFA NA UUNGWA MKONO WA DKT. SAMIA

Uteuzi wa Lukuvi pia unachukuliwa kama sehemu ya mkakati wa kitaifa wa CCM chini ya uongozi wa Mwenyekiti wake, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kuhakikisha chama kinapata ushindi mkubwa katika ngazi zote za uchaguzi – urais, ubunge na udiwani.

Ilani ya Uchaguzi ya CCM imeweka kipaumbele katika maeneo ya afya, elimu, miundombinu, kilimo na maji, na miradi hiyo ndiyo hasa inayotumika kama nyenzo ya ushindi katika majimbo mengi nchini. Lukuvi, akiwa na historia ya kusimamia utekelezaji wa miradi hiyo, anaingia kwenye kampeni akiwa na hoja thabiti za kuomba ridhaa ya wananchi.

Kwa wachambuzi wa siasa, Ismani inabaki kuwa miongoni mwa majimbo yenye mvuto kutokana na historia yake ya kisiasa na umuhimu wake katika siasa za Mkoa wa Iringa. Ushindi wa Lukuvi unatarajiwa kuimarisha zaidi nafasi ya CCM katika mkoa huo na kuongeza nguvu ya chama kuelekea uchaguzi wa mwaka huu.

Kwa kuchukua fomu hii, William Vangimembe Lukuvi ameanza rasmi safari yake ya kutetea kiti cha ubunge wa Jimbo la Ismani kwa tiketi ya CCM. 

Akiwa na historia ya uongozi thabiti, miradi mikubwa ya maendeleo na uungwaji mkono wa chama pamoja na wananchi, anaingia kwenye kinyang’anyiro cha uchaguzi mkuu akiwa na nafasi kubwa ya kuibuka mshindi.

Huku wananchi wa Ismani sasa wanabaki na jukumu la kufanya maamuzi kwa kura zao, lakini historia na kazi za Lukuvi ni kigezo kikubwa kinachoonyesha mustakabali wa jimbo hilo.

 Kwa mujibu wa kauli zake na mwenendo wa kampeni zinazoanza, inaonekana dhamira yake ni moja – kuendeleza kasi ya maendeleo na kuhakikisha Ismani inabaki kuwa ngome ya CCM na maendeleo endelevu.

Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI