Header Ads Widget

THOMAS NKOLA "MKULIMA" ACHUKUA FOMU ACT WAZALENDO KUGOMBEA UBUNGE..


Thomas Nkola maarufu mkulima(kushoto)akikabidhiwa fomu na Katibu ACT -Wazalendo jimbo la Maswa Magharibi,Emanuel Numbili(kulia)fomu ya kugombea ubunge jimbo la Maswa Magharibi.Thomas Nkola ‘Mkulima’ achukua fomu ACT Wazalendo.


Na Samwel Mwanga, Maswa


MWANAHARAKATI  mashuhuri Kanda ya ziwa,Thomas Nkola maarufu kwa jina la Mkulima, amechukua fomu ya kuomba kuteuliwa na chama cha ACT Wazalendo kugombea ubunge katika Jimbo la Maswa Magharibi.


Amekabidhiwa fomu hiyo leo jumamosi Mei 17,2025 na Katibu wa chama hicho jimbo la Maswa Magharibi,Emanuel Numbili katika mji wa Malampaka uliopo wilaya ya Maswa.


Akizungumza baada ya kuchukua fomu hiyo amesema dhamira yake kuu ni kutetea maslahi ya wakulima wa pamba ambao kwa muda mrefu, wamekuwa wakikandamizwa kwa kupata bei ndogo ya zao hilo licha ya juhudi kubwa wanazoweka.


Amesema kuwa amekuwa mwanaharakati kwa kupambania wananchi hasa wafugaji na wakulima na sasa ameamua mapambano hayo ayapeleke bungeni ili sauti ya wananchi iweze kusikika na serikali kuchukua hatua kwa vitendo vyote vya ubadhirifu vinavyofanywa na viongozi wa serikali.


Nkola amehoji uhalali wa viongozi waliopo sasa, hasa wabunge wanaotoka kwenye maeneo yanayolima pamba, kuendelea kuwa sehemu ya wafanyabiashara wa zao hilo, jambo alilolieleza kuwa ni mgongano wa maslahi unaowazuia kutetea wakulima ipasavyo.


“Haiwezekani mbunge awe mnunuzi wa pamba, halafu tumtarajie atang’ang’anie bei nzuri kwa wakulima,kwa sababu hiyo, wakulima hawawezi kupata haki yao kwenye soko la pamba,”


“Nimechukua fomu si kwamba nataka kugombana na mbunge aliyepo sasa,siasa zangu si za ugomvi,najua mbunge wetu hawezi kulisemea zao la pamba kutokana na wabunge walio wengi na viongozi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM)katika kanda ya ziwa na mkoa wa Simiyu wakiwemo, kujihusisha na biashara ya ununuzi wa zao hilo,”amesema.


Amesema kuwa na hivi karibuni atakwenda katika mahakama ya mkoa wa Simiyu kuwashtaki wabunge wote wa mkoa huo ambao wanajihusisha na biashara ya ununuzi wa zao la pamba kwani amegundua ya kuwa hao ndiyo wanaosababisha anguko la zao la pamba na kusababisha mkulima kutopata bei nzuri.


Ameongeza kusema kuwa mfumo wa sasa wa ununuzi wa pamba unawanyima wakulima nguvu ya kujadiliana kuhusu bei, huku baadhi ya viongozi wakitumia nafasi zao kunufaika binafsi.


Katibu wa ACT Wazalendo jimbo la Maswa Magharibi,Emanuel Numbili amesema kuwa wamejipanga kutetea wanyonge hasa wakulima wa zao la pamba kwani zao hilo kwa sasa linaendeshwa na viongozi waliopewa ridhaa na wananchi kwenda kuwasemea katika chombo cha kutunga sheria.


Maige Jilala mkazi wa Malamapaka amesema kuwa mji huo umekuwa na changamoto kubwa ya kuwepo kwa huduma za afya,barabara na maji licha ya kupewa ahadi za mara kwa mara huku wakikata tamaa ya kulima zao la pamba kutokana na bei kuwa ndogo.


“Nina imani iwapo Thomas Nkola atachaguliwa kuwa mbunge wa jimbo hili atasimamia hayo anayoyaeleza kutokana na jitihada anazizifanya za kupambania wanyonge na tumeona jinsi alivyoamua kuwashtaki baadhi ya wabunge mahakamani huyu ni mtetezi wa wanyonge,”amesema.


Naye Sosoma Ntobi mkazi wa mji wa Malampaka amesema kuwa mkulima wa zao la pamba kwa sasa ameachwa pekee yake hana mtetezi hivyo iwapo mtia nia huyo atachaguliwa itakuwa ni moja ya sauti ya watetezi wa zao hilo bungeni ili mkulima aweze kunufaika nalo tofauti na sasa.


Uchukuaji na urejeshaji wa fomu kwa nafasi za udiwani,ubunge na urais ndani ya ACT-Wazalendo utafungwa rasmi mei 28,2025.


MWISHO.


Thomas Nkola maarufu Mkulima akizungumza na wananchi wa mji wa Malampaka mara baada ya kuchukua fomu ya kugombea ubunge jimbo la Maswa Magharibi kupitia chama cha ACT-Wazalendo.


Baadhi ya vijana wa bodaboda waliojitokeza kumsindikiza Thomas Nkola maarufu Mkulima kwenda kuchukua fomu ya kugombea ubunge jimbo la Maswa Magharibi kupitia chama cha ACT-Wazalendo.







Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI