*Ni kuanzia Julai 2024, hadi Aprili 2025*
*Vibali 9,540 vya usafirishaji madini nje ya nchi vyatolewa*
*Matumizi ya Baruti yaongezeka*
WIZARA ya Madini kupitia Tume ya Madini imefanikiwa kukusanya jumla ya Shilingi 726,219,317,398.14 ambapo Shilingi 612,593,046,886.50 ni malipo ya mrabaha na Shilingi 113,626,270,511.64 ni malipo ya ada ya Ukaguzi.
Akizungumza Bungeni leo Mei 2, 2025 Waziri wa Madini Mheshimiwa Anthony Mavunde (MB) wakati akiwasilisha makadirio ya mapato na matumizi kwa mwaka wa fedha 2025/2026 amesema makusanyo hayo ni katika kipindi cha Julai 2024 hadi Machi 2025 ambapo madini yenye thamani ya Shilingi 11,376,270,882,758.50 yalizalishwa na kuiwezesha serikali kupata kiasi hicho cha fedha.
*USIMAMIZI, UKAGUZI NA BIASHARA YA MADINI*:
Waziri Mhe. Mavunde amesema katika kipindi cha Julai 2024 hadi Machi 2025, vituo vipya saba vya ununuzi wa madini vilianzishwa ambavyo ni Nhungwiza - Geita, Nachingwea, Liwale, Likofia - Lindi, Mugumu, Serengeti – Mara na Ikinabusu - Simiyu.
Mheshimiwa Mavunde amesema ongezeko hilo linafanya idadi ya vituo vya ununuzi wa madini kufikia 109.
Aidha, amesema katika kipindi husika, Wizara imeyatambua na kuzipa hadhi vituo vya ununuzi jumla ya maeneo 142 yanayotumika kufanyia biashara ya madini kwa wingi (bulk minerals) kupitia Gazeti la Serikali Na. 906 ya 15 Novemba 15, 2024.
Amesema, Tume ya Madini kwa kushirikiana na Mamlaka mbalimbali za Serikali ziliendelea kusimamia uendeshaji wa masoko na vituo vya ununuzi wa madini, kupitia usimamizi huo, kwa kipindi cha Julai 2024 hadi Machi 2025 mauzo ya shilingi 2,819,220,651,824.38 yalifanyika katika masoko ikilinganishwa na mauzo shilingi 1,930,698,791,589.30 yaliyofanyika katika kipindi cha Julai 2023 hadi Machi 2024.
“Kutokana na mauzo hayo, Serikali imekusanya kiasi cha shilingi 182,043,495,150.21 ikiwa ni tozo ya mrabaha na ada ya ukaguzi ikilinganishwa na Shilingi 136,731,358,413.41 zilizokusanywa katika kipindi kama hicho cha mwaka 2023/2024,”amesema Mhe. Mavunde.
*UTAMBUZI NA UTHAMINISHAJI WA MADINI*
Mheshimiwa Waziri Mavunde amesema kuwa Tume ya Madini imeendelea kusimamia shughuli za uchambuzi na uthaminishaji wa madini yote yaliyozalishwa na kutoa vyeti vya uthaminishaji wa madini pamoja na vibali vya usafirishaji na uingizaji madini.
Amesema, katika kipindi cha kuanzia Julai 2024 hadi Machi 2025, jumla ya vibali 9,540 vya usafirishaji madini nje ya nchi vilitolewa ikilinganishwa na vibali 8,809 vilivyotolewa katika kipindi kama hicho mwaka 2023/2024 huku thamani ya madini kwa vibali hivyo ni Shilingi 9,252,791,412,068.11.
Aidha, jumla ya vibali 116 vya uingizaji madini nchini vilitolewa ambapo madini yenye thamani ya dola za Marekani 14,813,664.38 yaliruhusiwa kuingia nchini.
*UKAGUZI WA HESABU ZA FEDHA NA KODI*
Waziri Mavunde amesema katika kipindi cha Julai 2024 hadi Machi 2025, Tume ya Madini imefanya ukaguzi kwa kampuni 21 za uchimbaji, miradi ya barabara na biashara ya madini.
Amesema, kati ya kampuni hizo, sita ni za uchimbaji madini ya dhahabu, 11 miradi ya barabara ambayo inatumia madini ujenzi, moja ni ya uchimbaji madini ujenzi, moja ni ya uchimbaji wa madini ya Almasi, moja ni ya umwagiliaji ambayo inatumia madini ujenzi na moja ni kiwanda cha kusafisha dhahabu.
Mhe. Mavunde amesema kaguzi hizo zimewezesha kuibua hoja mbalimbali zinazohusiana na kutolipwa kwa malipo ya Serikali shilingi 1,255,950,666.52. Kati ya fedha hizo, shilingi 576,917,781.17 zimelipwa baada ya ukaguzi. Kampuni tano zinazodaiwa shilingi 676,032,885.35 zimeahidi kuendelea kulipa deni kwa awamu.
“ Sambamba na hilo, Tume ya Madini imeendelea kufanya jitihada mbalimbali za kuhakikisha deni lote linalipwa kupitia vikao vya maridhiano na pale inapobidi kuchukua hatua kwa mujibu wa Sheria ya Madini Sura 123,”amesema.
*SHUGHULI ZA UKAGUZI WA MIGODI, MAZINGIRA NA USIMAMIZI WA BARUTI*
Aidha, amesema shughuli za Ukagauzi wa Migodi, Mazingira na Usimamizi wa Baruti, katika kipindi cha Julai 2024 hadi Machi 2025, migodi mikubwa saba ilikaguliwa, Migodi hiyo ni Dangote Cement Co. Ltd, Williamson Diamond Ltd, El-Hillal Minerals, North Mara Gold Mine, Geita Gold Mine, STAMIGOLD na Bulyanhulu Gold Mine.
“Kufuatia ukaguzi huo mapungufu mbalimbali yalibainika ikiwemo kutokuwepo kwa Mipango ya Ufungaji Mgodi (Mine Closure Plans), Mipango ya uchimbaji Madini (Mine Plans), kutokuwepo kwa maeneo maalum yaliyotengwa kwa ajili ya kuhifadhia miambataka (waste rock dumps), uwepo wa visima vya ufuatiliaji wa ubora wa maji (monitoring boreholes) vilivyoharibiwa kutokana na uvamizi pamoja na upanuaji wa mabwawa la topetaka. Migodi ilielekezwa kurekebisha mapungufu hayo na tayari wamerekebisha.,”amesema.
Amesema, ukaguzi katika Migodi ya Wachimbaji wa kati katika kipindi cha Julai 2024 hadi Machi 2025, jumla ya migodi 53 ya uchimbaji wa kati ilikaguliwa katika sehemu mbalimbali nchini.
Amesema, kaguzi hizo mapungufu mbalimbali yalibainika ikiwemo kukosekana kwa taarifa za usanifu wa maeneo ya kuhifadhi miambataka pamoja na mabwawa ya topetaka.
Waziri Mavunde amesema wahusika walielekezwa kurekebisha mapungufu yaliyojitokeza kwa kuzingatia Sheria ya Madini, Sura 123 na Sheria ya Usimamizi wa Mazingira, Sura 191 ambapo migodi husika imerekebisha mapungufu yaliyobainika.
Kwa upande wa ukaguzi katika Migodi ya Wachimbaji Wadogo, Waziri Mavunde amesema
katika kipindi cha Julai 2024 hadi Machi 2025, ukaguzi ulifanyika kwenye migodi ya wachimbaji wadogo 14,847 katika mikoa 30 ya kimadini nchini.
Amesema katika kaguzi hizo baadhi ya mapungufu yaliyobainika ni pamoja na kutofukiwa kwa mashimo ya uchimbaji yasiyotumika (abandoned pits), kutotumika kwa vifaa kinga, matumizi hafifu ya vifaa kinga na uhifadhi usio salama wa baruti na kukosekana kwa Mipango ya utunzaji wa mazingira (Environmental Protection Plan - EPP).
Amesema, wahusika walielekezwa kufanyia kazi mapungufu yaliyobainika ili kuwa na uchimbaji salama, endelevu na wenye tija.
*UKAGUZI WA MAGHALA, STOO NA MASANDUKU YA KUHIFADHIA BARUTI*
Mheshimwa Mavunde amesema, kuhusu ukaguzi wa Maghala, Stoo na Masanduku ya Kuhifadhia Baruti katika kipindi cha Julai 2024 hadi Machi 2025, jumla ya maghala 164, Stoo 268 na masanduku 207 yalikaguliwa katika mikoa yote ya kimadini.
Amesema, kaguzi hizo zilibaini uwepo wa mpangilio hatarishi wa vilipuzi, ukosefu wa leseni za uendeshaji wa maghala na kutokulipwa kwa ada za mwaka za leseni za maghala. Aidha, wahusika walirekebisha mapungufu hayo kama walivyoelekezwa.
*MAHITAJI YA BARUTI YAONGEZEKA*:
Waziri Mavunde amesema mahitaji na matumizi ya baruti kwa sasa yameongezeka kutokana na kuimarika kwa shughuli za uchimbaji wa madini na ujenzi wa miundombinu mbalimbali.
“Katika kipindi cha Julai 2024 hadi Machi 2025, vibali 267 vya kuingiza, kupitisha, kutengeneza na kuuza baruti nchini pamoja na vibali vya kusafirisha baruti nje ya nchi vimetolewa. Fedha zilizopatikana kupitia utolewaji wa vibali hivyo ni jumla ya dola za Marekani 133,438.,”amesema.
Aidha, amesema Tume ya Madini ilifanya ukaguzi kwenye maeneo yaliyoombewa kujengwa maghala ya kuhifadhi baruti ambapo maeneo yaliyofanyiwa ukaguzi ni Indo African Explosives Limited (Dar es salaam); Lindi Jumbo Limited (Lindi); AECI Mining Tanzania Ltd kwa mgodi wa Shanta Singida Gold Mine, Williamson Diamond Limited Shinyanga, Shanta New Luika Gold Mine Songwe; Ruvuma Coal Limited (Ruvuma); na East Africa Harmony Mining Co. Ltd (Tanga).
Amesema, ukaguzi huo ulibaini kuwa maeneo hayo yalikidhi matakwa ya Sheria ya Baruti, Sura 45 na hivyo kupewa vibali vya ujenzi wa maghala ya kuhifadhi baruti.
Pia, amesema Tume ya Madini imetoa vibali kwa ujenzi wa maghala ya kuhifadhia baruti ambapo maghala nane ni mapya ya kuhifadhi baruti yamejengwa na kampuni za Heshem Tanzania Co. Ltd (Chunya), China Civil Engineering Construction Corporation (Nzega), Ideal Detonators Tanzania Limited (Pwani), Canuck Company Limited (Kahama), Sekenke One Mining Cooperative Society Limited (Singida), Esap Mining Services Limited (Songwe) na Tianpin (T) Investment Management Limited (Kahama). Aidha, maghala hayo yatasaidia katika utoaji wa huduma za uchimbaji katika maeneo husika.
0 Comments