Na Matukio Daima.
MBEYA.Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Dkt. Juma Zuberi Homera, amekutana na Mabalozi wa Tanzania waliopo katika nchi mbalimbali barani Afrika kwa lengo la kuangazia fursa za uwekezaji kati ya mkoa wa Mbeya na nchi wanazowakilisha. Miongoni mwa masuala yaliyogusiwa ni pamoja na maboresho ya miundombinu ya usafirishaji ikiwemo barabara, reli ya TAZARA, bomba la mafuta na uendelezaji wa bandari kavu.
Mkutano huo umewakutanisha Balozi wa Tanzania nchini DRC, Said Mshana; Balozi Agnes Kayola wa Malawi; Balozi Mathew Mkingule wa Zambia; Balozi Mdogo Magabilo Murobi wa Lubumbashi pamoja na Afisa Biashara kutoka Zambia, John Ngowo. Ujio wao mkoani Mbeya ni sehemu ya kushiriki katika Maonesho ya Kibiashara ya Mbeya Expo 2025.
Dkt. Homera aliwaeleza mabalozi hao kuwa mkoa wa Mbeya umetenga maeneo maalum kwa ajili ya uwekezaji kama vile Tanganyika Packers na eneo la TBC, huku akiweka wazi mwaliko kwa wawekezaji kutoka nchi jirani kuja kuwekeza katika sekta mbalimbali. Alibainisha pia kuwa miradi kama ya ujenzi wa mji wa kisasa katika Kata ya Nsalala na ukamilishaji wa barabara ya njia nne itachochea zaidi ukuaji wa uchumi wa mkoa.
Akitaja mazao ya kimkakati yanayolimwa mkoani humo kama kakao, parachichi, mpunga, tumbaku, pareto, chai na kahawa, Dkt. Homera alisema kuna nafasi kubwa ya kuwekeza kupitia kilimo. Kwa upande wao, mabalozi walionesha utayari wa kuwasilisha taarifa hizo kwa wawekezaji katika nchi wanazowakilisha ili kukuza ushirikiano wa kibiashara na maendeleo.
0 Comments