Na Gabriel Kilamlya Matukio Daima NJOMBE
Mwenge wa uhuru wa Mwaka huu umehitimisha mbio zake mkoani Njombe Leo kwa kutembelea Jumla ya miradi saba yenye thamani ya zaidi ya sh. Bilioni 2.5 ya halmashauri ya mji wa Njombe huku ukitoa maagizo mbalimbali kwa viongozi wa Chama na Serikali.
Akizungumza wakati wa kupokea Mwenge huo kutoka Halmashauri ya Wilaya ya Ludewa, Mkuu wa Wilaya ya Njombe Juma Sweda ameitaja miradi hiyo kuwa ni pamoja na kukagua msitu wa Ilonganjaula, kugawa mizinga 20 ya nyuki kwenye kikundi na kuzindua madarasa sita shule ya sekondari Mpechi sambambamba na kuzindua mradi wa gari la Miradi ya Maendeleo la Halmashauri hiyo.
Ukiwa katika kata ya Mjimwema umezindua huduma za mionzi kwenye kituo Cha Afya huku Diwani wa kata hiyo Nestory Mahenge akisema changamoto ya ukosefu wa huduma ya mionzi ilikuwa ikiwafanya Wananchi wake kutumia gharama kubwa kwenda kuzipata katika Hospitali za Kibena,Rufaa na hata Ikonda jambo ambalo kwa sasa imetatuliwa.
Naye Mwenyekiti wa Halmashauri ya mji wa Njombe Erasto Mpete amesema Vifaa vya mionzi vimeletwa kwa Zaidi ya shilingi Milioni 200 huku kituo Cha Afya Mjimwema kikitumia Zaidi ya shilingi Milioni 600 kupitia mapato ya ndani hivyo wananchi wanapaswa kunufaika nacho na kukitunza.
Akizindua huduma ya mionzi katika kituo hicho pamoja na kugawa vyandarua kwa wananchi katika kituo hicho Kiongozi wa mbio za Mwenge wa uhuru Kitaifa Mwaka huu Ismail Ali Ussi amesema huduma zilizoanza kutolewa kwa wananchi ni Bora kwani azma ya Rais Samia Suluhu Hassan ni kuona Afya za watanzania Zinaboreka.
Aidha Ussi amewataka wananchi kutumia kituo Cha Afya kwa ajili ya Afya zao badala ya kwenda kuwasumbua wataalamu wa Afya Wala kuwakejeli.
Kwa upande wake wakazi wa kata ya Mjimwema Mjini Njombe wamesema hivi sasa wanafurahia kupata huduma zote katika kituo hicho Cha Afya kilichojirani tofauti na hapo awali.
Mei 9 mwenge wa uhuru unakabidhiwa Madaba mkoani Ruvuma baada ya kukimbizwa mkoani Njombe na kupitia miradi 62 yenye thamani ya Zaidi ya Shilingi bilioni 17.
0 Comments