MKOA wa Lindi unatarajiwa kuwa lango kuu la uchimbaji wa madini kutokana na kuonekana kuwa na aina zaidi ya 10 za madini mbalimbali yanayopatikana kwa wingi ikiwemo madini ya kimkakati kama Kinywe (Graphite) na Nickel.
Akizungumza katika mahojiano maalum, Afisa Madini Mkazi wa Mkoa wa Lindi, Mhandisi Emmanuel Shija amesema utafiti uliofanywa na Taasisi ya Jiolojia na Utafiti wa Madini Tanzania (GST) mwaka 2024 kwa kutumia ndege nyuki umebaini uwepo wa kiasi kikubwa cha madini mkakati ya Kinywe katika eneo la Ruangwa katika Mkoa wa Lindi. Aina nyingine za madini yanayotambuliwa kuwepo ni pamoja na madini yenye asili ya Chuma, kama Nickel, Dhahabu, Shaba, Manganese pamoja na Madini ya viwandani ambayo ni Jasi, Chokaa, Chuma na Chumvi.
Mhandisi Shija amesema pia Mkoa wa Lindi unazalisha kwa wingi madini ya viwandani ya Gypsum ambayo yanatumika zaidi kwenye viwanda vya saruji na gypsum board vilivyopo ndani ya nchi na nchi jirani.
“Mkoa wa Lindi kwa sasa tunautambulisha kama ‘The Future Mineral Hub of Tanzania' (kitovu cha uchimbaji madini Tanzania). Pamoja na kutokuwa na miradi mingi mikubwa kwa sasa ni mategemeo yetu kuwa ndani ya miaka michache ijayo tunategemea kuwa na miradi mikubwa ya madini ndani ya mkoa wetu. Hii ni kutokana na ukweli kuwa kuna upatikanaji wa madini mbalimbali kwa kiwango kikubwa amesema Mhandisi Shija.
Amesema, kwa sasa upo mradi wa uchimbaji wa kati wa Lindi Jumbo ambao umeanza kuzalisha madini ya kinywe yenye ubora wa hali ya juu kwa ajili ya matumizi ya betri na vifaa vya kielektroniki.
“Hali ya uzalishaji ni nzuri kwenye makusanyo tuna aina kuu tatu za madini zenye mchango mkubwa, ambazo ni Nickel yanaongoza kwa kuchangia asilimia 35 ya makusanyo, lakini pia tuna madini ya Dhahabu yanayochangia asilimia 30 yakifuatiwa na madini ya Gypsum yenye mchango wa asilimia 20.
Aidha, Mhandisi Shija amesema katika mwaka wa fedha wa 2024/2025 walipangiwa kukusanya jumla ya Shilingi za kitanzania Bilioni 7.5 na wamekamilisha lengo la makusanyo ya maduhuli hayo tangu Mei 5 mwaka huu.
“Mpaka sasa tumeshakusanya shilingi Bilioni 7.9 sawa na asilimia 105 ya lengo tulilopangiwa na Serikali,”amesema Shija.
Amesema kuwa mwaka ujao wa fedha 2025/2026 wameongezewa lengo kwa kupangiwa kukusanya Shilingi Bilioni 10.5 na mategemeo yao kwa mwenendo uliopo wa ukuaji wa sekta ndani ya mkoa watafanikiwa kulifikia lengo hilo.
0 Comments