Na Ashrack Miraji Matukio Daima App
Mkuu wa Wilaya ya Handeni, Mhe. Japhari Kubecha, amefanya kikao kazi maalum na wakuu wa taasisi mbalimbali zinazotoa huduma ndani ya wilaya hiyo, akisisitiza umuhimu wa ushirikiano wa karibu katika kuharakisha maendeleo ya wananchi.
Taasisi zilizoshiriki kikao hicho ni pamoja na Wakala wa Barabara Vijijini na Mijini (TARURA), Wakala wa Usambazaji Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA), Wakala wa Huduma za Misitu (TFS), Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA), Mamlaka ya Hali ya Hewa (TMA), Chuo cha Maendeleo ya Wananchi na Kituo cha Uendelezaji Madini.
Katika hotuba yake, Mhe. Kubecha aliwapongeza viongozi hao kwa kazi nzuri wanayoifanya lakini pia akawataka kuongeza ubunifu, uwajibikaji na kasi ya utendaji ili kukidhi matarajio ya wananchi. “Wananchi wetu wanatarajia huduma bora, za haraka na zenye tija. Hili linawezekana iwapo tutakuwa wamoja na kushirikiana bila mipaka,” alisema DC Kubecha.
Aidha, alisisitiza kuwa changamoto nyingi zinazowakabili wananchi zinaweza kupatiwa ufumbuzi wa haraka iwapo taasisi zote zitakuwa na mfumo wa kushirikiana taarifa na kupanga kwa pamoja mikakati ya utekelezaji. Alibainisha kuwa mwelekeo wa sasa serikalini ni kufanya kazi kwa kushirikiana, si kila taasisi kujitenga kivyake.
Katika kikao hicho, baadhi ya wakuu wa taasisi walipata fursa ya kuwasilisha mafanikio na changamoto zinazowakabili katika utekelezaji wa majukumu yao, huku wakiahidi kushirikiana kwa karibu na ofisi ya mkuu wa wilaya katika mipango yote ya maendeleo.
Mkutano huo unatajwa kuwa ni sehemu ya mkakati wa Mkuu wa Wilaya kuimarisha uwajibikaji, uwazi na utekelezaji wa mipango ya maendeleo kwa ushirikiano wa wadau wote muhimu katika wilaya ya Handeni.
0 Comments