Kesi ya uhaini inayomkabili Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Taifa Tundu Lissu imeendelea tena leo, Jumanne Mei 06.2025 kwa ajili ya kutajwa
Akizungumza mbele ya Mahakama katika kesi hiyo inayoendelea kwa njia ya mtandao Wakili wa Serikali Mwandamizi Tawabu Yahya amesema upelelezi wa kesi hiyo bado haujakamilika hivyo kuiomba Mahakama kuhairisha hadi tarehe nyingine
Hata hivyo, taarifa hiyo imeonekana kutopokelewa vyema na Mawakili wa utetezi wakiongozwa na Wakili Mpale Mpoki ambapo wameieleza Mahakama hiyo kuwa hawafurahishwi kwa namna upande wa Jamhuri unavyochelewesha upelelezi wa shauri hilo, hivyo kutumia hadhara hiyo kuomba kupatiwa maelezo ya kina ni kipi hasa kinakwamisha upelelezi wa shauri hilo ambalo tangu mwanzo ilielezwa kuwa ushahidi wake uko kwenye mtandao wa YouTube
Upande wa Jamhuri kupitia kwa Wakili wa Serikali Mwandamizi Tawabu Yahya uliieleza Mahakama kuwa hakuna kifungu chochote cha sheria kinachowalazimisha kueleza nini kimesalia kwenye upelelezi, badala yake alitumia fursa hiyo kuieleza Mahakama kuwa pindi upelelezi wa shauri hilo utakapokamilika wataweka taarifa zake kwenye mfumo 'mtandao' sambamba na kuwapatia Mawakili wa utetezi
Hoja kubwa iliyowasilishwa na Mawakili wa utetezi Mahakamani leo kuhusiana na shauri hilo ni kwamba upelelezi ukamilike kwa wakati ili shauri hilo likasikilizwe Mahakama Kuu kama inavyotakiwa, kwani kuchelewesha kufanya hivyo ni kutomtendea haki mteja wao
Baada ya kusikiliza hoja za pande zote mbili, Hakimu Mkazi Mwandamizi Godfrey Mhini anayesikiliza shauri hili alitoa wito kwa upande wa Jamhuri kuhakikisha wanaharakisha upelelezi na kwamba tarehe inayofuata shauri hilo kutajwa wahakikishe waeleze hatua iliyofikiwa, baada ya kueleza hayo akaahirisha shauri hilo hadi Mei 19.2025 kwa ajili ya kutajwa
Hata hivyo, mtuhumiwa wa kesi hiyo Tundu Lissu aliendelea kugoma kushiriki shauri hilo kwa njia ya mtandao, na badala yake Mkuu wa Gereza Ukonga Kamishna Msaidizi wa Magereza Juma Mwaibako alisema alipowasiliana na mshtakiwa amegoma kusikiliza shauri hilo kwa njia ya mtandao.
MWISHO.
0 Comments