Header Ads Widget

JKT YAWAITA VIJANA WALIOMALIZA KIDATO CHA SITA 2025

 

Na Hamida Ramadhani, Matukio Daima App – Dodoma

Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) limewataka vijana wote waliomaliza Kidato cha Sita mwaka 2025 kutoka shule za Tanzania Bara kuripoti kwenye makambi maalum ya mafunzo ya kijeshi kwa mujibu wa Sheria, kuanzia Mei 28 hadi Juni 8, mwaka huu.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa kwa waandishi wa habari jijini Dodoma na Kaimu Mkuu wa Tawi la Utawala, Kanali Juma Mlay, kwa niaba ya Mkuu wa JKT, Meja Jenerali Rajabu Mabele, amesema mafunzo hayo ni sehemu ya maandalizi ya vijana kiuzalendo, kinidhamu na kimaadili kabla ya hatua nyingine za maisha.

Kanali Mlay amefafanua kuwa vijana wamegawanywa katika makambi mbalimbali nchini. Baadhi ya makambi hayo ni JKT Rwamkoma (Mara), Msange (Tabora), Ruvu na Kibiti (Pwani), Mpwapwa na Makutupora (Dodoma), Mafinga (Iringa), na Mlale (Ruvuma).

Aidha, makambi mengine ni Mgambo na Maramba (Tanga), Makuyuni na Orkjoro (Arusha), Bulombora, Kanembwa na Mtabila (Kigoma), Itaka (Songwe), Luwa na Milundikwa (Rukwa), pamoja na JKT Nachingwea (Lindi), hivyo vijana wanatakiwa kufuatilia kwa makini kambi walizopangiwa.

Akizungumzia maandalizi ya kuripoti kambini, Kanali Mlay amesema vijana wanapaswa kufika wakiwa na vifaa maalum ikiwemo bukta ya Dark Blue yenye mpira kiunoni, isiyo na zipu, yenye mfuko mmoja nyuma, T-shirt ya kijani, track suit ya kijani au blue, pamoja na raba zenye rangi zinazofanana.

Vifaa vingine ni shuka mbili za rangi ya blue bahari, soksi ndefu nyeusi, nguo za kuzuia baridi kwa waliopangiwa kambi zilizo kwenye mikoa yenye baridi, pamoja na nyaraka muhimu kama vyeti vya kidato cha nne na sita, cheti cha kuzaliwa, na nakala zinazohitajika kwa udahili wa elimu ya juu.

Nauli ya kwenda kambini na kurejea nyumbani pia ni moja ya mahitaji muhimu ambayo vijana wanatakiwa kuandaa kabla ya tarehe ya kuripoti.

Kwa mujibu wa Kanali Mlay, orodha rasmi ya majina ya waliochaguliwa pamoja na kambi walizopangiwa, mkoa na wilaya, inapatikana kwenye tovuti ya JKT: www.jkt.mil.tz. Kupata taarifa hizo, kijana anapaswa kuingiza jina au namba ya shule aliyohitimu Kidato cha Sita.

“Mara atakapoingiza jina la shule, ataona sehemu iliyoandikwa ‘waliochaguliwa’. Akibofya hapo, ataweza kuona jina lake na taarifa kamili za kambi aliyopangiwa,” alieleza Kanali huyo huku akisisitiza umuhimu wa kufuata maelekezo kwa umakini.

Mwisho

Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI