NA MATUKIO DAIMA MEDIA
matukiodaima4@gmail.com
0754026299
Sherehe za Siku ya Wafanyakazi Duniani (Mei Mosi) mwaka huu zilizofanyika kitaifa mkoani Singida zimeacha gumzo kubwa kutokana na ubunifu ulioonyeshwa na waandaaji, hususan kwa kuingiza mashindano ya mbio za magari kama sehemu ya burudani ya sherehe hizo.
Tukio hili la kitaifa lilihudhuriwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, ambaye alikuwa mgeni rasmi, na uwepo wake ulileta hamasa kubwa miongoni mwa wananchi na wafanyakazi kutoka maeneo mbalimbali ya nchi.
Tofauti na miaka mingine, mwaka huu sherehe hizo zilipambwa kwa namna ya kipekee ambayo haijazoeleka. Ingawa kila mwaka Mei Mosi huwa ni siku ya kipekee kwa wafanyakazi kusherehekea mafanikio na kuwasilisha changamoto zao kwa serikali, ubunifu wa mwaka huu umeonyesha mwelekeo mpya wa jinsi ambavyo tukio la kitaifa linaweza kuwa na mvuto wa aina yake.
Wafanyakazi pamoja na kujazwa na Shangwe ya hotuba ya Rais kuhusu masuala ya nyongeza ya mishahara bado Shangwe hizo zilisindikizwa na mbio kali za magari zilizofanyika pembeni ya sherehe hizo, na hivyo kuongeza upekee wa tukio hilo.
Ubunifu huo wa kuongeza mashindano ya magari katika sherehe hizo ni jambo la kupongezwa sana Mkuu wa Mkoa wa Singida, Halima Dendego, pamoja na kamati yake ya maandalizi, wameonyesha mfano bora wa jinsi ya kuongeza mvuto kwenye matukio makubwa ya kitaifa.
Wameweza kuonesha kuwa Siku ya Wafanyakazi si lazima iwe ya hotuba na maandamano pekee, bali pia inaweza kuwa siku ya burudani, mashindano na michezo, ambayo huleta watu pamoja na kuongeza ushiriki wa jamii kwa ujumla.
Kwa kawaida, ujio wa Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan huwa ni kivutio kikubwa kwenye matukio ya kitaifa.
Kutokana na namna anavyosikilizwa na kupendwa na wafanyakazi na wananchi kote nchini , hasa kutokana na msimamo wake wa kuimarisha maslahi ya wafanyakazi.
Kauli yake kuhusu nyongeza ya mishahara mwaka huu ilikuwa ni kilele cha sherehe hiyo, lakini mashindano ya magari yaliyoandaliwa yameongeza ladha ya tukio hilo na kufanya Mei Mosi ya mwaka huu kuwa ya kipekee isiyosahaulika kirahisi.
Hali ya amani, ushiriki wa wananchi kwa wingi, pamoja na maandalizi bora yalionyesha dhamira ya mkoa wa Singida kuifanya siku hii kuwa ya kukumbukwa.
Kwani kutokana na tukio hili lilivyoandaliwa, ni wazi kuwa Mei Mosi inaweza kuwa zaidi ya tukio la kawaida la kisiasa na kiserikali inaweza kuwa pia jukwaa la kuonesha vipaji, ubunifu, michezo na burudani ambayo huleta pamoja watu wa makundi mbalimbali.
Hakika ni jambo la kupongeza Tena mkoa wa Singida umeandika historia mpya kwenye maadhimisho ya Mei Mosi mikoa mingine kubeba ubunifu huu na kutumia katika Matukio ya kimkoa na Kitaifa.
0 Comments