Header Ads Widget

DC KUBECHA AAHIDI USHIRIKIANO IMARA NA MRADI WA BOMBA LA MAFUTA HANDENI


Na Ashrack Miraji Matukio Daima App 

Handeni, Mei 22, 2025 – Mkuu wa Wilaya ya Handeni, Mheshimiwa Japhet Kubecha, amefanya kikao kazi na timu ya wataalamu kutoka mradi wa bomba la mafuta ghafi Afrika Mashariki (East African Crude Oil Pipeline – EACOP), katika eneo la mradi lililopo wilayani humo.

Kikao hicho muhimu kilihudhuriwa pia na Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya pamoja na wataalamu mbalimbali kutoka katika mradi huo. Lengo kuu la kikao lilikuwa ni kujitambulisha kwa timu ya mradi kwa uongozi wa wilaya na kutoa taarifa kuhusu maendeleo ya utekelezaji wa shughuli za mradi huo hadi sasa.

Katika hotuba yake, Mheshimiwa Kubecha aliipongeza timu hiyo kwa kufika kujitambulisha rasmi na kutoa taarifa ya maendeleo ya mradi. Alisisitiza kuwa Wilaya ya Handeni iko tayari kutoa ushirikiano wowote unaohitajika ili kuhakikisha mradi huo mkubwa unatekelezwa kwa mafanikio na kukamilika kwa wakati.


Mradi huu ni wa kimkakati na una manufaa makubwa kwa taifa letu na jamii ya Handeni kwa ujumla. Serikali ya Wilaya iko tayari kushirikiana nanyi kwa karibu ili kuona tunafanikisha lengo hili,” alisema DCKubecha.

Aidha, alitoa wito kwa wananchi wa maeneo yanayopitiwa na mradi huo kuendelea kutoa ushirikiano kwa wakandarasi na wataalamu wanaotekeleza mradi, huku akisisitiza umuhimu wa kulinda miundombinu na mali za mradi kwa manufaa ya wote.

Katika kikao hicho, wataalamu wa EACOP walieleza hatua zilizofikiwa katika utekelezaji wa kazi mbalimbali, zikiwemo tathmini ya mazingira, usajili wa mali, fidia kwa wakazi walioguswa na mradi, na maandalizi ya ujenzi wa miundombinu ya bomba hilo.


Walisema kuwa lengo ni kuhakikisha ujenzi unaanza kwa wakati huku wakizingatia viwango vya kimataifa vya usalama, mazingira, na uwajibikaji kwa jamii.

Kikao hicho kilimalizika kwa makubaliano ya kuanzishwa kwa kamati ndogo ya ufuatiliaji kati ya ofisi ya mkuu wa wilaya na timu ya mradi ili kurahisisha mawasiliano na kushughulikia changamoto zinazoweza kujitokeza wakati wa utekelezaji.


 

Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI