Na Shomari Binda-Musoma
WAKALA wa Barabara "TANROADS" mkoa wa Mara imefanikisha kupitika kwa barabara inazozihudumia licha ya mvua zinazoendelea kunyesha.
Mkuu wa mkoa wa Mara Kanali Evans Mtambi amesema kufanikisha huko kumetokana na kazi nzuri ya usimamizi unaofanywa na Meneja wa TANROADS mkoa wa Mara mhandisi Vedastus Maribe.
Akiwasilisha utekelezaji wa ilani ya uchaguzi ya CCM ya mwaka 2020/2025 kwenye kikao cha Halmashauri Kuu ya mkoa wa Mara leo mei 22,2025.kenyw ukumbi wa chama hicho wa mkoa amesema kupitika kwa barabara hizo kwa kipindi chote kumesaidia kuinua uchumi wa wananchi wa mkoa wa Mara.
Amesema TANROADS mkoa wa Mara katika kipindi cha miaka mine ya Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan imepokea kiasi cha bilioni 240.9 ambazo zimetekeleza miradi mbalimbali.
Kanali Mtambi amesema kwenye mtandao wa barabara wa kilometa 893 ni kilometa 11 peke ambazo zina shida kidogo na zinaendelea kushughulikiwa.
Amesema mradi wa barabara ya Tarime-Nyamongo hadi Serengeti yenye urefu wa kilometa 35.05 wenye thamani ya bilioni 34.6 upo kwenye asilimia 56 na unaendelea kutekelezwa.
Barabara ya Kisorya-Nyamswa umekamilika na wananchi wakiitumia kwa shughuli za kiuchumi na usafirishaji huku mzani unaopima magari yakiwa yanatembea uliopo Bunda wenye thamani ya bilioni 22 nao umekamilika.
Mkuu huyo wa mkoa amesema katika kuzungumzia masuala ya miundombinu ya barabara amesema barabara ya Mika-Utegi-Kirongo ilikuwa ikijengwa kwa kusuasua na ingechukua muda mrefu kukamilika kwake lakini kwa sasa serikali inasukuma kwa kasi iweze kukamilishwa.
" Ipo barabara ya Musoma- Makojo-Busekera mkandarasi ameshapatikana na ujenzi wake utaendana na ujenzi wa daraja la Suguti litakalojengwa kwa fedha za benki ya dunia.
" Barabara zetu zimepitika kwa muda wote licha ya mvua zinazoendelea kunyesha kutokana na usimamizi mzuri unaofanywa na TANROADS",amesema.
Katika uwasilishaji huo wa ilani licha masuala ya barabara mkuu huyo wa mkoa wa Mara amewasilisha pia miradi ya elimu,afya,maji,kilimo,umeme na masuala ya kijamii ambayo yametekelezwa kwa ufanisi mkoa wa Mara.
Mwenyekiti wa CCM mkoa wa Mara PatrickChandi amesema Kamati ya Siasa imefanya ziara na kukagua miradi 38 ambayo utekelezaji wake umekamilishwa kwa asilimia 100.
Amesema kutokana na utekelezaji huo Chama cha Mapinduzi kunakwenda kushinda kwa kishindo kwenye uchaguzi wa 2025.
0 Comments