Kamati ya Siasa ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Mbeya Vijijini Mei 13, 2025 imeendelea na ziara yake ya ukaguzi wa miradi ya maendeleo kama ambavyo ilani ya Chama cha Mapinduzi inaelekeza.
Kamati hiyo ikiongozwa na Katibu wa CCM Wilaya ya Mbeya vijijini (kichama) Rehema Mpagike kwa niaba ya Mwenyekiti wa Wilaya Hakimu Sebastian Mwalupindi, ameongoza wajumbe wa kamati hiyo kutembelea na kukagua vikundi viwili vya wanawake wanaonufaika na mikopo ya asilimia 10 wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbeya.
Katibu Rehema amevipongeza vikundi hivyo ambavyo ni Tusehaje kilichopo Kata ya Isuto kikijihusisha na uuzaji wa pembejeo za kilimo na hadi sasa kinaendelea kujiimarisha kiuchumi na wanatarajia kuanzisha biashara nyingine kutokana na faida walioipata.
Katibu huyo amekitaja kikundi kingine kuwa ni Vayuwa kilichopo katika kata ya Ilembo ambao wanajihusisha na uuzaji wa mazao ya nafaka pamoja na vyakula vya kuku ambapo ameipongeza pia Halmashauri ya Mbeya kwa kuhakikisha mikopo hiyo inanufaisha wananchi.
Pia kamati ya siasa Mbeya vijijini imepitia miradi ya usambazaji umeme vijijini (REA) na wakala wa usambazaji maji vijijini (RUWASA) ambapo imepongeza juhudi za viongozi hasa wa kuchaguliwa na wataalam kwa kuendelea kusimamia miradi hiyo wakiongozwa na mkuu wa wilaya ya Mbeya Mhe. Beno Malisa kwa ufuatiliaji na usimamizi wa miradi hiyo pamoja na Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Mbeya na kuhimiza uwajibikaji huo uwe endelevu kwa manufaa ya wananchi.
0 Comments