Kocha mpya wa Brazil Carlo Ancelotti amesema anajivuniakuiongoza timu bora zaidi duniani” na analenga kushinda kombe la Dunia la 2026
Kocha huyo mwenye umri wa miaka 65 alitangazwa kuwa mkufunzi mpya wa Brazil katika mkutano na waandishi wa habari katika makao makuu ya shirikisho la soka la Brazil (CBF).
Raia huyo wa Itali anajiunga na timu ya Brazil kwa jina maarufu Selecao baada ya kuwa meneja wa Real Madrid kwa muda wa miaka minne iliyopita. Ameshinda Ligi ya Mabingwa mara tatu na taji la La Liga mara mbili akiwa kocha wa klabu hiyo.
Ancelotti pia aliiongoza AC Milan kuwa mabingwa wa Ulaya mara mbili, alishinda Ligi ya Premia na Kombe la FA akiwa na Chelsea pamoja na mataji ya Ufaransa na Ujerumani akiwa na Paris St-Germain na Bayern Munich mtawalia.
“Nina kazi kubwa mbele yangu,” alisema. “Nimefurahia, changamoto ni kubwa. Nimekuwa na uhusiano maalum na timu hii. Tutafanya kazi ili kuifanya Brazil kuwa bingwa tena.”
“Ninajivunia kuiongoza timu bora zaidi duniani.”
Brazil wameshinda Kombe la Dunia mara tano, na ushindi wa hivi karibuni zaidi ulikuwa mwaka 2002, na mchezo wa kwanza wa Ancelotti na wao ni mechi mbili za kufuzu kwa Kombe la Dunia.
0 Comments