Shirika la kutetea haki za binadamu la Amnesty International limesema kuwa kundi la waasi wa March 23 Movement (M23) limewaua, kuwatesa na kuwashikilia baadhi ya mateka huku wakiwaweka katika mazingira ya kinyama kwenye maeneo ya kizuizini huko Goma na Bukavu mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo (DRC).
"Vitendo hivyo vinakiuka sheria za kimataifa za kibinadamu na vinaweza kuwa uhalifu wa kivita," Amnesty International ilisema.
Ripoti iliyotolewa na shirika hilo inasema kati ya Februari na Aprili 2025, ilihoji raia 18 waliokuwa wafungwa - wanaume wote - ambao walishikiliwa kinyume cha sheria katika maeneo ya kizuizini na M23 huko Goma na Bukavu, tisa kati yao waliteswa na wapiganaji wa M23.
Kulingana na taarifa ya shirika hilo, ngozi iliyojivisha kundi la waasi la M23 ya kuleta amani mashariki mwa DRC, ni njia ya kuficha maovu wanayotenda dhidi ya wale wanaoamini kuwa wanaenda kinyume na matakwa yao.
Shirika hilo limetoa wito wa kundi hilo kuwaachiliwa wale wanaowashikilia mateka mara moja na kwamba wanastahili kuonyesha ubinadamu kwa kila wanayemzuia na wawaruhusu kuwa na mawakili na familia zao.
0 Comments