NA MATUKIO DAIMA MEDIA
CHAMA cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania (TAMWA) kinatarajia kutoa tuzo za uandishi wa habari za maendeleo inazofahamika kama Samia Kalamu Awards kwenda kwa waandishi 79 walioshinda katika makundi makuu matatu
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam leo Mkurugenzi Mtendaji wa Tamwa, Dk. Rose Reuben alisema kwa kushirikiana na Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), wanatangaza rasmi kufanyika kwa utoaji wa tuzo hizo utakaongozwa na Rais Dk. Samia Suluhu Hassan APrili 29, mwaka huu.
“Samia Kalamu Awards ni tuzo zinazohusisha habari za maendeleo katika makundi makuu matatu, kundi la kwanza linahusisha tuzo za kitaifa ikiwamo tuzo ya chombo cha habari mahiri kitaifa.
“Tuzo nyingine ni za wanahabari wabobevu, tuzo ya Afisa Habari Mahiri wa Serikali, Tuzo ya Mwandishi wa Habari Mahiri Kitaifa na Tuzo ya Uandishi wa Habari za Matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia”amesema na kuongeza.
Akifafanua zaidi kuhusu makundi ya tuzo, alisema kundi la pili, Tuzo kwa vyombo vya Habari ambazo ni, Tuzo za Televisheni, Vyombo vya Habari Mtandaoni, Redio ya Kitaifa, Magazeti na Redio za Kijamii.
Alisema kundi la tatu, Tuzo za kisekta zitakazotolewa kwa waandishi wa habari waliobobea katika kuandika Makala za Maendeleo kwenye sekta mbalimbali ikiwamo afya, maji, nishati, mazingira,jinsia wanawake na makundi maalum, ujenzi, viwanda na biashara, maliasili na utalii, mifugo na uvuvi, uchumi wa buluu, kilimo,utamaduni, sanaa na michezo, TEHAMA na ubunifu, mazingira, ardhi na makazi, madini, fedha na uchumi, vijana, elimu na uwekezaji.
“Tamwa na TCRA tunatoa wito kwa waandishi na vyombo vyote vya habari nchini kushiriki kikamilifu katika kuhamasisha hafla hii ya kihistoria ambayo inatoa nafasi kwa wanahari kutangaza mchango wao kwa jamii na taifa kwa ujumla” alisema Dk. Rose.
Mwisho
0 Comments