Na Fadhili Abdallah, Kigoma
WAKULIMA wa kahawa katika jimbo la Buhigwe wilaya ya Buhigwe mkoani Kigoma wameitaka serikali kuanzisha kituo cha uuzaji wa kahawa (MNADA) katika wilaya hiyo ili kuondokana na mpango wa kuuza kahawa yao katika mnada wa Moshi mkoani Kilimanjaro unaosimamiwa na bodi ya kahawa nchini (TCB).
Wakulima hao wakiongozwa na diwani ya kata ya Mwayaya Abel Mlala walitoa kilio hicho mkutano wa Mbunge wa jimbo la Buhigwe, Felix Kavejuru aliyefanya mkutano wa hadhara kijijini hapo ambapo wakulima hao walimtaka mbunge huyo kusaidia mpango wa kuwepo kwa kituo cha kuuzia kahawa (Mnada) katika maeneo yao ili kuondokana na kutegemea kuuza kahawa hiyo kwenye mnada wa Moshi mkoa Kilimanjaro.
Akiunga mkono kauli ya diwani Mlala, mkulima mwingine Pascal Kababaye alisema kuwa kuwepo kwa mnada wa kuuzia kahawa katika wilaya yao kutawaongezea idadi kubwa ya wanunuzi na kusimamia bei hivyo kahawa itakuwa na faida kubwa kwao kuliko wanavyo fanya sasa wanapotegemea kuuza kahawa yao katika soko la Moshi mkoani Kilimanjaro.
Kwa upande wake Mkulima Juliana Baranzira alimweleza mbunge huyo kuwa pamoja na kutaka mnada wa kuuzia kahawa kwenye wilaya yao lakini pia wana changamoto kubwa ya kuchelewa kwa mbolea ya ruzuku sambamba na gharama kubwa ya madawa ya kunyunyizia wadudu ambayo hayana ruzuku hivyo wananunua kwa wafanyabiashara hivyo kuiomba serikali kuweka ruzuku kwenye madawa ya kunyunyizia wadudu ya zao la kahawa.
Akizungumza katika mkutano huo Mbunge wa jimbo la Buhigwe Felix Kavejuru amewataka wakulima wa kahawa katika jimbo kuongeza uzalishaji sambamba na kuzingatia ubora ili kuwezesha serikali kutekeleza mpango wa kuweka mnada wa zao hilo wilayani humo.
Kavejuru alisema kuwa ili kuwezesha kutekelezwa kwa mpango wa kupatikana kwa mnada wa kahawa katika wilaya ya Buhigwe na mkoa Kigoma kwa jumla jambo la msingi ni wakulima kuwa na kiwango kikubwa na cha kutosha cha kahawa ambayo inakusudiwa kuuzwa nje lakini pia kahawa hiyo iwe imezingatia vigezo vya ubora katika uaandaaji wake kwa soko la kimataifa.
Sambamba na hilo Mbunge huyo alisema kuwa ataendelea kuwasiliana na watendaji wa serikali na wizara ya kilimo ili kuwezesha mbolea ya ruzuku inapatikana kwa wakati sambamba na kupigia kelele upatikanaji wa pembejeo za kahawa ikiwemo madawa ya kupulizia kwa bei ya ruzuku ili kupunguza mzigo kwa wakulima katika kuandaa zao hilo.
0 Comments