Mkurugenzi mtendaji wa mamlaka ya maji safi na usafi wa mazingira Mbeya (Mbeya UWSA) CPA Gilbert Kayange, ametembelea kiwanda cha kuzalisha mabomba ya chuma yatakayotumika kusafirisha maji kutoka kwenye mradi wa chanzo cha maji mto Kiwira hadi Mbeya mjini na maeneo mengine.
CPA Kayange amefanya ziara hiyo jijini Dar es Salaam akiambatana na mhandisi mshauri wa mradi wa maji wa mto Kiwira (GkW Consult Ltd) na mkandarasi mjenzi (China Railway Construction Engineering Company Ltd) ambao kwa pamoja wametembelea kiwanda hicho cha kuzalisha mabomba ya chuma cha Tanzania Steel Pipes (TSP) Dar es Salaam, lengo kuu likiwa ni kuhakiki viwango vya ubora wa bomba zitakazotumika kusafirisha maji katika mradi wa maji kutoka chanzo cha maji cha mto Kiwira.
Kwa mujibu wa mamlaka ya maji safi na usafi wa mazingira Mbeya, bomba hizo ni za kipenyo cha milimita 1,200 na zina uwezo wa kukidhi kwa ubora kusafirisha maji kutoka kwenye mradi hadi kufika kwa wananchi.
Kwa mujibu wa uongozi wa Kiwanda cha TSP, uzalishaji wa mabomba unaendelea vizuri na unazingatia viwango vyote vya ubora kwa maendeleo zaidi.
Ikumbukwe kuwa mradi wa maji kutoka chanzo cha mto Kiwira unatekelezwa na Mamlaka ya maji safi na usafi wa mazingira Mbeya na utakapokamilika unatarajiwa kuzalisha maji kiasi cha lita Milioni 117 kwa siku hatua itakayosaidia kuongeza hali ya upatikanaji wa maji kwa wananchi wa jiji la Mbeya na maeneo mengine ya jirani kwa zaidi ya asilimia 95.
0 Comments