Header Ads Widget

VIONGOZI,WANACHAMA CHADEMA SINGIDA WAANGUA KILIO OFISINI KUMLILIA LISSU

 

Na Matukio Daima Media, Singida 

VIONGOZI na wanachama wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Mkoa wa Singida wameangua kilio katika ofisi za chama hizo zilizopo eneo la Ngurudoto kata ya Majengo Manispaa ya Singida wakimlilia Mwenyekiti wao wa Taifa, Tundu Lissu.


Viongozi na wanachama hao waliangua kilio hicho juzi wakati Askofu Mwanamapinduzi, Hezekia Wenje, akiwaelezea kesi ya uhaini aliyofunguliwa Lissu adhabu yake inaweza kuwa ni kunyongwa hadi kufa.


"Kesi aliyofunguliwa Mwenyekiti wetu Lissu adhabu yake itakuwa ni kunyongwa hadi kufa, lakinj sisi tuliopo tusiogope tuendeleze mapambano ya No Reform No Election hakuna kukata tamaa," alisema Wenje ambaye ya kueleza hivyo vilio vilianza kutawala katika ofisi za chama hicho.


Naye Mwenyekiti wa Chadema Mkoa wa Singida, Omari Toto,aliitaka Serikali, Jeshi la Polisi na CCM kumuachia Lissu haraka iwezekanvyo bila hivyo watahakikisha wanapigana mpaka tone la mwisho la damu.


"Hatupo tayari kuona ndugu yetu anateswa kihuni kwa ajili ya mambo ya kisiasa Lissu ni ndugu yetu wanasingida tumpiganie hadi aachiwe maana hajafanya kosa lolote na kama ni suala la No Reform No Election lilikuwa ni azimio la Baraza Kuu na Mkutano Mkuu wa Chadema sio suala la Lissu kama Lissu," amesema Toto.


Toto alisisitiza kuwa serikali na CCM watambue kuwa uchaguzi hautafanyika na wala sio utani maana Chadema ina wafuasi wengi ambao watakusanya nguvu nchi nzima kuhakikisha wanazuia uchaguzi," alisema Toto.


"Haya yote yanayoendelea katika nchi yetu ni kujidhalilisha maana tunafahamu Lissu wanampa kesi kubwa ya uhaini ili kupoza suala la No Reform No Election mimi nawaambia suala la No Reform No Election  lilo pale pale tutaendelea nalo hadi mwisho," amesisitiza Toto.


Naye Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Kanda ya Kati, Jackison Kingu, amemuomba Rais Dk.Samia Suluhu Hassan, kuingilia kati ili Mwenyekiti wa Taifa wa chama hicho,Tundu Lissu aweze kuachiwa.

Akizungumza katika mkutano wa hadhara uliofanyika stendi ya zamani ya mabasi mjini Singida, amesema Lissu atakapoachiwa Chadema itakaa meza moja kujadiliana ili kama itawezekana chama hicho nacho kiweze kushiriki Uchaguzi Mkuu utakaofanyika mwaka huu.


"Nimuombe Rais Dk.Samia kupitia mkutano huu mimi ambaye ni Lissu ni ndugu yangu tunatoka wote Wilaya ya Ikungi kama ataona vyema amuachie Lissu ili aje ajadiliane mambo ambayo hayaendi sawa kwa maslaha mapana ya taifa hili ambalo limekuwa na historia ya kuwa na amani na utulivu," amesema Jingu. 

Aidha, Jingu alimuomba aliyekuwa Mwenyekiti wa taifa wa Chadema, Freeman Mbowe,aingie kati asaidie Lissu aachiwe na kusahahu  mitifuano na kukashifiana kulikojitokeza wakati wa uchaguzi ndani ya chama.

"Pamoja na maneno ambayo wamekashifiana,Lissu amekutana na madhila haya nimuombe Freema Mbowe yeye ambaye anafahamika katika taifa hili na jumuiya zingine hiki kilichomkuta Lissu ana haki kuingilia kati aende akamuone mwenzake wakashauriane namna iliyo njema," alisema.


MWISHO

Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI