Na Shemsa Mussa -Matukio Daima
Kagera.
Kwa kipindi cha miaka miwili Mifumo hiyo imewasaidia wakulima na wamehamasika Kwa kiasi kikubwa na Kupata faida ikiwemo uwepo Wa bei nzuri,ubora Wa zao na Kupata Malipo Kwa wakati.
Hayo yameelezwa na Mrajisi wa vyama vya ushirika katika zao la kahawa mkoani Kagera Bi Enikia Bisanda, amesema matumizi ya teknolojia katika sekta ya kahawa yameanza kuleta tija kwa wakulima, hususan kupitia matumizi ya mizani ya kidijitali, mfumo wa stakabadhi ghalani na mauzo ya moja kwa moja kwa wanunuzi.
Akizungumza na Chombo hiki Mrajisi huyo Bi Enikia, amesema kuwa mizani ya kidijitali imesaidia kuondoa malalamiko ya wakulima kuhusu upotevu wa uzito wa kahawa wakati Wa mauzo , na kuongeza uwazi na haki katika mchakato wa upimaji wa mazao.
“Faida nyingine ya mfumo huu ni kuboresha ubora wa kahawa,na pia mfumo huu wa stakabadhi ghalani umewawezesha wakulima wengi kupeleka mazao yako katika AMCOS ambapo Kahawa inahifadhiwa katika mazingira salama na kuhakikiwa ubora wa kahawa na mwishowe kupelekwa mnadani. Kwa maana hiyo kahawa ya Kagera unaweza kushindana vyema katika soko la kimataifa,” amesema Bi Enikia.
Kuhusu mauzo ya moja kwa moja,kuna baadhi ya vyama vya ushirika 13 mbavyo vinauza moja kwa moja kwa mnunuzi kwa mikataba maalum ambayo inasimamiwa na mamlaka husika. VYama hivi pia vinatumia mizani ya kidigitali katika upimaji wa kahawa pale ambapo mkulima ameleta kahawa yake kwenye AMCOS.
Vile vile amesema Mizani hiyo inasomeka kwenye Mfumo wa usimamizi wa vyama vya Ushirika ambapo Kila msimamizi anaona taarifa moja kwa moja ya chama killichokusanya kahawa na taarifa hizo zinaenda mnadani kwa ajili ya kuuzwa. Ameongeza Bi Enikia.
Mrajisi huyo amesema serikali kwa kushirikiana na vyama vya ushirika imekuwa ikiendesha mafunzo kwa viongozi wa vyama vya ushirika pamoja na wakulima ili kuhakikisha wanakuwa na uelewa wa kutosha kuhusu mifumo hiyo na kuitumia kwa manufaa ya wanachama wote.
Pia ametoa wito kwa wakulima kujiunga na vyama vya ushirika ili waweze kunufaika na fursa zilozopo kwenye ushirika, akibainisha kuwa ushirikiano kati ya serikali, vyama na wakulima ni msingi imara wa kuinua uchumi wa mkulima mmoja mmoja na taifa kwa ujumla.
0 Comments